Simba hakuna presha tena...!



MABAO matatu aliyotupia wavuni mshambuliaji mpya wa Yanga, Malimi Busungu kwenye michuano ya Kombe la Kagame kabla ya jana Jumapili, yameitetemesha Simba iliyo kambini visiwani hapa.
Makocha wa Simba wameshtushwa na maendeleo ya haraka aliyoanza kuyapata Busungu akiwa na Yanga. Kocha Msaidizi wa Simba Suleiman Matola amemsifu straika huyo akidai kuwa ni moja ya mastraika hatari Simba iliyowakosa kwenye usajili.
“Kuna Busungu (Malimi) halafu kuna Kaseke (Deus), hawa jamaa ni hatari sana na moto wao ndiyo huu wanaouonesha kwenye Kagame. Ni aina ya wachezaji waliopo Yanga ambao iwapo wangejiunga na Simba wangekuwa bora zaidi,” alisema Matola.
“Wapo vizuri sana wanajua, wanafunga na wana kasi nzuri, hata hivyo Simba na sisi tunawengi wazuri na wenye uwezo wa juu. Naamini Ligi itakapoanza watu wataweza kujionea zaidi jinsi wanavyofunga.
“Kuna Kiiza (Hamisi), Ajibu (Ibrahim), kuna Mgosi (Mussa Hassan), Maguli (Elius) na wengine. Kwanini tushindwe?”alihoji Matola.
Hata hivyo, Matola alijifariji kuwa baada ya kiungo Mwinyi Kazimoto kutua Simba, mambo yatakuwa bambam akisema: “Tumepata bonge la kiungo anayekuja kutuongezea nguvu katikati.
“Kwa aina ya uchezaji wake naamini atakuwa msaada mkubwa kwenye kikosi cha Simba kwa msimu ujao.”

No comments