KITANUKA TAIFA
AZAM na Yanga zinapokutana huwa na ushindani na upinzani mkali kiasi wachezaji wao kufikia kukunjana mashati.
Bahati mbaya ni kwamba wawakilishi hao wa Tanzania keshokutwa Jumatano watavaana kwenye robo fainali ya Kombe la Kagame, ikiwa ni mwezi mmoja kabla ya kukutana tena kwenye mechi ya Ngao ya Hisani kwa ajili ya kuzindua msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2015-2016.
Ingawa mashabiki wengi wa soka hakupenda timu hizo zikutane katika robo fainali itakayoanza kesho Jumanne, lakini bao la Mrundi Amissi Tambwe dhidi ya Al Khartoum ya Sudan ndilo lililoamua timu hizo zikutane mapema zaidi katika michuano hiyo ya Kagame.
Mashabiki wengi walipenda timu hizo angalau zikutane hatua ya nusu fainali au fainali ili kupata burudani na kuiwezesha Tanzania kama wenyeji kuwa na nafasi ya kubakisha taji, lakini matokeo yaliyopatikana jana Jumapili pale Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, yamewahisha mambo.
Tambwe aliifungia Yanga bao tamu la kichwa katika dakika ya 30 ya mchezo ambao alikosa mabao mengi ya wazi.
Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi 9 na kukamata nafasi ya pili nyuma ya Gor Mahia iliyoishinda Telecom 3-1 mapema jana.
Gor Mahia imekuwa vinara wa Kundi A ikiwa na pointi 10 na Al Khartoum iliyokuwa ikiongoza kabla ya mechi za jana imeshuka hadi nafasi ya tatu ikiwa na pointi saba.
Msimamo wa kundi hilo jinsi ulivyo umeipa nafasi Yanga kuvaana na Azam iliyoongoza Kundi C. Timu hizo zilipokutana mara ya mwisho katika Ligi Kuu, Yanga ililala 2-1. Mechi yao wawakilishi hao inarejesha pambano la fainali za Kagame la mwaka 2012 ambapo Yanga iliitambia Azam mabao 2-0.
Kocha wa Azam, Stewart Hall alikakariwa mapema kuwa licha ya kujua kukutana na Yanga ni mtihani mgumu kwao, lakini wamejiandaa kupambana wafike nusu fainali.
Al Khartoum: Mohamed Ibrahim, Amin Ibrahim, Hamza, Daoud, Salaheldin Merghani, Wagdi Awad, Anthony Akumu, Domenic Abui, Atif Khalif/ Ismaila Baba, Badreldin Eldoon/Marwan Salih, Ahmed Adam.
Yanga: Ally Mustafa ‘Barthez’, Joseph Zuttah, Oscar Joshua/Mwinyi Mngwali, Pato Ngonyani, Kelvin Yondani/Nadir haroub ‘Cannavaro, Mbuyu Twite, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Malimi Busungu na Andrey Coutinho/ Geofrey Mwashiuya
Post a Comment