Huyu Mganda atawanyoosha
KOCHA wa Coastal Union, Jackson Mayanja, amekerwa na kitendo cha wachezaji waliosajiliwa kuchelewa kuwasili na amewapa siku tatu kuhakikisha wameripoti klabuni.
Amelalamika kwamba kuchelewa kuwasili kwa wachezaji wengi hadi juzi Ijumaa kumeathiri mipango na mazoezi yanayoendelea kwenye Uwanja wa shule ya Sekondari Popatlal Jijini Tanga.
“Kabla ya kuingia kwenye ligi nina programu ya kwanza kuwaweka pamoja kisaikolojia wakiwa kambini, kuwafundisha fomesheni ninayotaka ichezwe mashindanoni na kisha kuwapeleka nchini Kenya kucheza michezo minne ya majaribio na timu kubwa zikiwamo Sofapaka na Bandari ya Mombasa,” alisema kocha huyo raia wa Uganda.
“Labda nieleze wazi kwamba mwaka huu natarajia kikosi changu kilete ushindani mkubwa hata wa kutwaa ubingwa lakini msimu wa mwakani tutakuwa tunaingia kuleta taji Tanga na si vinginevyo,”alibainisha Mayanja.
Hata hivyo Meneja wa klabu hiyo, Akida Machai, kuhusiana na suala la wachezaji kuchelewa, alisema: “Wachezaji wengine wamewasili na wote watakuwa wamewasili kuungana wenzao muda wowote. Baada ya timu kukamilika tutahamishia kambi mjini Korogwe.
“Huko tunaamini timu itakuwa imetulia kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.”
Post a Comment