KIPA wa Simba, Ivo Mapunda, atakaa nje kwa wiki mbili bila kufanya mazoezi ya aina yoyote huku akiendelea kupata matibabu kutokana na ugonjwa mpya unaomkabili wa kusumbuliwa na nyama za paja.
Ivo alipata majeraha hayo akiwa kambini Lushoto ambako timu hiyo ilipiga kambi ya wiki mbili hivyo viongozi wa Simba walilazimika kumrudisha jijini Dar es Salaam siku mbili kabla ya timu kurejea na alianza matibabu kwa Dk. Gilbert.
Ivo ameliambia Mwanaspoti kuwa hajawahi kusumbuliwa na tatizo la nyama za paja na hii ni mara yake ya kwanza ila anaamini atakuwa fiti baada ya matibabu hayo na kufuata masharti aliyopewa.
“Nafikiri hii ni kutokana na kufanya mazoezi sana kwani awali nilikuwa nikifanya mazoezi kwenye kituo cha kocha Manyika, tulikuwa tukifanya mazoezi magumu halafu nilienda kukutana na mazoezi mengine magumu Lushoto,” alisema.
“Katika maisha yangu ya soka sijawahi kusumbuliwa na misuli ya paja, lakini nilishangaa nikiwa kambini kupatwa na tatizo hili, kwa sasa naendelea na matibabu na nimeambiwa nipumzike wiki mbili ndipo nitaanza mazoezi naamini nitakuwa vizuri tu.”
Kwa sasa Simba ipo jijini Dar es Salaama na huenda ikaenda Zanzibar kwa ajili ya kambi ya kujiandaa na mechi yao ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya AFC Leopards ya Kenya siku ya kilele cha Simba Day na endapo Simba wataenda Zanzibar basi Ivo hatakuwemo kwenye msafara huo.
Gari la Kiiza lasukumwa
Mashabiki wa soka juzi Jumamosi walilazimika kulisukuma gari la straika mpya wa Simba, Hamis Kiiza ‘Diego’ huku wakimshangilia kwa furaha baada ya kutomwona kwa kipindi kirefu.
Mashabiki hao walionekana bado wanamkubali Kiiza kwa soka lake alipokuwa Yanga na walianza kulisukuma gari hilo kuanzia sehemu aliyokuwa ameligesha mpaka usawa wa geti la kutokea pale Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Yanga ilipocheza na Gor Mahia katika fungua dimba ya Kombe la Kagame.
Kiiza aliachwa na Yanga wakati wa usajili wa dirisha dogo msimu uliopita na sasa amesajiliwa na Simba kwa mkataba wa miaka miwili hivyo ataanza kuonekana tena uwanjani hapo kuanzia msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Kiiza alifika Taifa akiwa na wachezaji wenzake wa Simba kuangalia mechi hiyo ingawa muda wote alikaa na timu ya KCCA ya Uganda.
Akizungumza na Mwanaspoti baada ya mechi hiyo Kiiza alisema: “Timu zote zimecheza vizuri lakini Yanga (waliolala 2-1) hawakuwa na bahati ya kufunga kwani walipata nafasi lakini hawakuzitumia vizuri.”
Post a Comment