Milioni 500 za Yanga zipo wapi?


Kocha wa Yanga, Mzungu Hans Van Pluijm
TUNAFUNGWAJE? Ni swali ambalo matajiri wa Yanga waliokuwa kwenye jukwaa kuu waliulizana baada ya timu yao kupachikwa bao la pili pale Uwanja wa Taifa juzi Jumamosi mbele ya Gor Mahia.
Hawakuamini macho yao, lakini kocha Hans Pluijm akawaambia tulieni huku tajiri mwingine akiwakumbusha kwamba hata mwaka 1993 kule Kampala, Uganda SC Villa iliifunga Yanga mabao 2-1 katika mchezo wa ufunguzi na Yanga hiyo hiyo ikadunda mpaka fainali ikaja kukutana na Villa hao hao ikawafunga mabao 2-1 na kupeleka taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) Jangwani.
Kabla ya mchezo huo wa juzi, Yanga ilifanya maandalizi ya maana ikiwamo kucheza mechi nne za kirafiki na kwenda kuificha timu katika eneo la jeshi ili wapinzani wao washindwe kuiba mbinu, lakini mambo yalionekana kwenda mrama kwenye mechi hiyo ya ufunguzi wa Kagame.
Mbali na maandalizi hayo, Yanga pia ndiyo timu yenye kikosi ghali zaidi nchini na wachezaji wake ndiyo wanaolipwa ghali zaidi ukiachilia mbali wale wa Azam ambayo inamilikiwa na Bilionea, Said Salim Bakhresa.
Kikosi cha Yanga cha wachezaji 11 kilichoanza dhidi ya Gor Mahia Jumamosi gharama yake ni Sh570.9 milioni ikiwa ni fedha za usajili pekee achilia mbali nyota wengine waliokuwa benchi. Katika kikosi hicho mchezaji ghali zaidi ni kiungo Haruna Niyonzima aliyepewa mkataba mpya wa Sh 117.9 milioni hivi karibuni.
Hiyo juzi ilikuwa kama balaa kwa Yanga ambapo straika wake, Donald Ngoma, ambaye usajili wake umeigharimu Yanga dola 50,000 (zaidi ya Sh100 milioni) alikitolewa nje kwa kadi nyekundu ndani ya dakika 25 tu za mwanzoni. Ngoma ndiye aliyesababisha bao la kufutia machozi la Yanga.
Habari kutoka Kenya zinaeleza kuwa kikosi cha Gor cha wachezaji 11 kilichoanza juzi dhidi ya Yanga kimegharimu kiasi cha Sh8 milioni kwa fedha za Kenya ambapo kwa hapa Tanzania ni sawa na Sh164 milioni.
Wachezaji waliosajiliwa kwa gharama kubwa kwenye kikosi cha Gor ni Khalid Aucho aliyesajiliwa kwa dau la dola 20,000 (Sh41 milioni) akitokea Tusker pia ya Kenya. Mwingine ni Meddie Kegere alipewa mkataba wa dola 15,000 (Sh30.5 milioni) wakati Abouba Simomana na Karim Nigiyimana waliosajiliwa kutoka Rayon Sports ya Rwanda mara baada ya michuano ya Kagame mwaka jana walipewa dau la dola 10,000 (Sh 20.5 milioni) kila mmoja.
Straika Michael Olunga aliyeifunga Yanga mabao yote mawili juzi, alisajiliwa kwa dau la dola 5,000 (Sh 10 milioni) akitokea Thika United ya nchini humo.
Hii inamanisha kwamba gharama za kikosi chote cha Gor ni manunuzi ya wachezaji wawili tu pale Yanga. Ni manunuzi ya Niyonzima Sh 117 milioni na Deus Kaseke Sh 35 milioni.
Usajili wa Gor uliofanywa mwezi Januari mwaka huu ambao unatajwa kuigharimu timu hiyo kati ya Sh 6-7 milioni za Kenya, ni pamoja na kipa Boniface Oluoch kutoka Tusker.
Wachezaji wengine ni Nizigiyimana na Sibomana kutoka Rayon Sports ya Rwanda, Kagere kutoka FK Tirana ya Albania, Aucho kutoka Tusker, Innocent Wafula kutoka Chemelil Sugar, Ali Abondo kutoka Tusker, Olunga na Dirkir Glay kutoka Thika United.

No comments