Simba yasajili jembe kuivuruga Yanga


NI Michael Olunga? Hapana! Simba imemuweka kwenye faili lake kiungo mkabaji wa Gor Mahia, Aucho Khalid ambaye juzi Jumamosi aliivuruga Yanga kwenye mechi ya ufunguzi ya Kombe la Kagame.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa Aucho ana nafasi kubwa ya kusajiliwa Msimbazi na tayari mazungumzo baina ya viongozi wa klabu hizo yameanza ingawa viongozi wengine wa usajili wa Mnyama wameshauri kwamba jina hilo lihifadhiwe, waangalie wachezaji wengine zaidi kwa vile bado wana muda.
Straika wa Gor Mahia, Olunga, ndiye aliyeifungia timu yake mabao yote katika ushindi wa 2-1 kwenye mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, bao la Yanga likiwa ni la kujifunga kwa mabeki wa Gor Mahia katika harakati za kuokoa shuti lililopigwa na Donald Ngoma, ndipo beki Dirkir Glay akajifunga.
Kutokana na kasi ya Olunga na shida ya Simba ya kusaka straika katika kipindi hiki cha usajili, wengi walidhani vigogo hao watashawishika na Olunga lakini wao wamesema hapana ila anayezungumziwa kwao ni kiungo mkabaji Aucho ambaye ni raia wa Uganda.
Hata hivyo, Simba hawawezi kumng’oa Olunga kwani ana mkataba wa miaka minne na timu yake ingawa inasemekana pia kuwa Wekundu hao wamevutiwa na kiwango cha kipa wa Gor Mahia, Boniface Oluoch ambaye amewataka viongozi wa Simba kwenda kuzungumza na viongozi wake.
Habari kutoka ndani ya Simba, zinasema kuwa juzi Jumamosi wakati mechi hiyo ikiendelea vigogo wa Simba walioongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe, walifuatilia mechi hiyo ingawa Olunga alionyesha kiwango cha juu lakini hawana mpango naye kwani tayari wamemnasa Laudit Mavugo.
Tayari viongozi wa Simba walitamka kuwa watatumia michuano hiyo kupata wachezaji wapya wenye sifa na kiwango cha juu kujaza nafasi za wachezaji wa kigeni. Nafasi hizo ni za Emmanuel Okwi (aliyeuzwa Denmark) na Raphael Kiongera (majeruhi).
Mpaka sasa inao wachezaji wanne wa kigeni; Hamisi Kiiza, Simon Sserunkuma, Juuko Murshid na Laudit Mavugo.

No comments