Simba yampandia dau beki wa Yanga SC
SIMBA wajanja sana aisee, kwani wameamua kupitia mlango wa nyumba na sasa inataka kuwazidi ujanja watani zao Yanga baada ya kutangaza dau la Sh40 milioni kukamilisha usajili wa beki wa kati wa Mtibwa Sugar, Salum Mbonde.
Awali Simba walimtangazia mchezaji huyo dau la Sh20 milioni na kupotezewa ndipo Yanga walipoibuka kumtaka kwa dau kubwa zaidi, lakini safari hii Simba imeamua kumtega Mbonde kwa kumwambia watampa dau hilo jipya.
Ingawa Yanga nao baada ya kupata taarifa kuwa mama mzazi wa Mbonde anayeitwa, Tatu Kiroboto alitarajiwa kutua Dar es Salaam leo Alhamisi, wakafanya michakato ya kukutana naye kwa mazungumzo zaidi.
Lakini Simba inayofanya michakato ya usajili huo kwa siri ili Yanga wasigundue mipango yao, inaweza kupiga bao la usajili huo kimya kimya ili kuboresha kikosi chao msimu ujao.
Mwenyekiti wa Usajili wa Simba, Zacharia Hanspoppe alishamwita mama huyo jijini Dar es Salaam kwa mara ya kwanza kwa gharama zake, wakafanya mazungumzo yaliyoshindwa kutoa mwafaka.
Jamaa wa karibu wa Mbonde aliliambia Mwanaspoti kuwa Simba kupitia kwa Hans Poppe walikuwa tayari kutoa Sh20 milioni kiwango ambacho mama huyo aliyeachiwa majukumu yote ya usajili na Mbonde aliyepo Afrika Kusini kwenye mashindano ya Cosafa na Taifa Stars, alikikataa.
Lakini jana Jumatano, Simba walimpigia tena simu na kutamka wapo tayari kutoa Sh 40 milioni ili kukamilisha usajili huo na mama amekubali.
“Tatu amekubali kupokea Sh40 milioni za Simba, lakini akawaambia azungumze kwanza na mtoto wake ili kujua watakamilishaje zoezi hilo, unajua Mbonde anamtegemea mama yake kwa kila kitu, atakachokiamua mama ndiyo atafanya,” alisema rafiki huyo wa Mbonde.
“Lakini Yanga nao waliposikia mama huyo anakuja Dar es Salaam, waliwasiliana naye na ahadi yao, leo hii (Alhamisi) akutane na Katibu wa Yanga (Jonas Tibohora) ili wazungumze.”
Mwanaspoti ilimtafuta, Tatu ili kufahamu undani wa sakata hilo alisema: “Kama nilivyosema awali, nazungumza na timu zote Simba, Yanga na Azam na naangalia ipi itakubaliana na sisi. Kweli kabisa leo (jana) nitakuwa Dar es Salaam lakini safari yangu ni ya kifamilia.”
“Namsindikiza mwanangu (dada yake Mbonde) anakwenda masomoni Marekani, masuala mengine mimi siyajui,” alisema.
Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alipoulizwa alijibu kwa ufupi kuwa dirisha la usajili bado halijafunguliwa.
Post a Comment