Heh! Yanga sasa mmezidi



YANGA imetenga dau la Sh797 milioni ili kusuka kikosi kipya ambacho kitadumu kwa misimu miwili ijayo na kufanya vizuri zaidi kwenye michuano ya kimataifa kuanzia na Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
Katika msimu uliomalizika ilitumia karibu Sh500 milioni tu.
Tayari katika kiasi hicho, zimeshapungua fedha zilizotumika kwenye usajili wa nyota wawili wa kigeni Mbuyu Twite na Haruna Niyonzima.
Jopo la usajili wa Yanga limepania kusuka kikosi ambacho kitakuwa imara zaidi na ambacho kitakuwa na mtazamo mpya na tayari Mwenyekiti wa klabu ambaye ni Bilionea Yusuf Manji ameunga mkono.
Habari za ndani ambazo Mwanaspoti imejiridhishwa nazo, zinasema kwamba usajili wa Yanga umepanga kunasa wachezaji wote wa maana wa ndani yakiwemo majina yaliyopendekezwa kama viungo Haruna Chanongo ambaye ni huru na Deus Kaseke wa Mbeya City.
Fungu hilo la Yanga litatumika pia kwenye maandalizi ya kambi kwa ajili ya Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa, tayari imefahamika kwamba Niyonzima amechukua dola 60,000 (Sh120 milioni) katika mkataba wake wa miaka miwili huku pia Twite akichukua dola 30,000 (Sh60 milioni) akisaini mkataba wa mwaka mmoja.

No comments