Hesabu zaibeba Simba nafasi ya pili
KOCHA wa Simba, Goran Kopunovic amesema hesabu zinaibeba timu
hiyo katika mbio za kuwania nafasi ya pili ambapo amezitaja mechi mbili
dhidi ya Mbeya City na ile na Azam kuwa ndiyo zimeshikilia tiketi yao ya
kupanda ndege.
Azam imeonekana kutetereka katika mechi mbili
zilizopita baada ya kutoa sare na Mbeya City na kisha Mtibwa hivyo
kusalia katika nafasi ya pili na pointi 38 baada ya kucheza mechi 20
wakati Simba inashika nafasi ya tatu na pointi 35 baada ya mechi 21.
Kopunovic ambaye timu yake iliifunga Toto Africa
mabao 3-0 katika mchezo wa kirafiki juzi Jumamosi jijini Mwanza, alisema
sasa timu yake imerejea rasmi katika mbio za nafasi ya pili.
Hata hivyo alisema wanatakiwa kushinda mechi zote tano kama wanahitaji nafasi hiyo.
Hesabu zipo hivi; Sasa Simba inatakiwa kuiombea
njaa Azam ipoteze mechi mbili halafu Simba iibuke na ushindi katika
mechi baina yao ili Azam ishindwe kufikisha pointi 49 ambazo Simba
itafikisha kama itashinda michezo yote hiyo.
Endapo Azam itafanikiwa kushinda michezo mitatu na
kupata sare moja katika michezo yake sita iliyosalia itakuwa
imeiondosha Simba rasmi katika mbio za nafasi hiyo ya pili kwani
watafikisha pointi 49 ambapo pia timu hiyo ina wastani mzuri wa mabao ya
kufunga na kufungwa.
Hata hivyo rekodi zinaonekana kuibeba Azam kwani
katika mechi nne za mwisho zilizozikutanisha timu hizo, Azam imeshinda
mara mbili na nyingine mbili zilimalizika kwa sare.
Post a Comment