Yanga wapata winga mpya wa ukweli
BAADA ya mshambuliaji mpya wa Yanga,Geofrey Mwashiuya kufanya mazoezi ya wiki moja na kikosi hicho, kocha Hans Pluijm amefunguka na kutamka ni mchezaji wa ukweli na atamchezesha winga ya kushoto.
Lakini Mwashiuya akatoboa siri nzito kwa kusema,
alikataa pesa za Simba, Azam zilizokuwa zinamwania hapo awali na kusaini
Yanga kwa sababu alikuwa anaipenda tangu utotoni.
Pluijm aliliambia Mwanaspoti: “Nimemwangalia
mazoezini naweza kusema ni mchezaji mzuri ambaye ana kila kitu. Ni
kijana mdogo ambaye anatakiwa apewe muda na atakuja kuisaidia vizuri
Yanga hapo baadaye kikubwa ajitambue.”
“Na kutokana na staili yeke, nitamtumia kucheza
winga ya kushoto, hapo ndipo mahali pake,”alisema Pluijm. Kwa upande wa
Mwashiuya ambaye alisajiliwa na Yanga kwa mkataba wa miaka mitatu
akitokea Kimondo ya Mbozi mapema mwaka jana alisema: “Sifichi, niliamua
kuja kuichezea Yanga kwa sababu ya mapenzi. Naipenda Yanga tangu
nilipokuwa mtoto mdogo.”
“Na siku nilipopigiwa simu kuwa wananihitaji,
nilifurahi sana, kwani kama siyo mapenzi, ningeweza kusaini Simba au
Azam hapo awali, walinifuata nisaini kwao,”alisema Mwashiuya.
Akizungumzia ushindani ndani ya kikosi hicho,
Mwashiuya alisema: “Ushindani upo mkubwa, mimi ni mgeni kwenye timu
nahitaji muda, lakini ninachoahidi ni kuwapa raha ile wanayoitaka
mashabiki na wapenzi wa klabu hii, kikubwa wanipe muda.”
Mwashiuya ametua Yanga ambako atawania namba na
mawinga wengine kama, Mrisho Ngassa, Simon Msuva, Mbrazil Andrey
Coutinho na Nizar Kharfan.
Kwa upande wa Pluijm alisema: “Mwashiuya ni kijana
mdogo, lakini ni mchezaji ambaye amekamilika kwa kila kitu na uhakika
akiendelea hivi, ataisaidia timu hapo baadaye.”
“Kutokana na staili yake, kama kocha nitamtumia kucheza winga ya kushoto,”alisema Pluijm.
Post a Comment