Simba walianzisha tena.. Ni hatari hii.....
KABLA ya dirisha la usajili Ligi Kuu Bara msimu ujao halijafunguliwa tayari vurugu mechi ndani ya Simba na Yanga zimeanza.
Ndani ya Simba imeelezwa tayari imeshapokea mapendekezo tofauti kutoka kwa viongozi wa klabu hiyo kuhusu usajili huo.
Kwa kawaida utaratibu wa usajili wa timu unafanywa
na Kamati ya Ufundi kutokana na mapendekezo ya makocha lakini
kinachofanyika sasa Simba ni kila kiongozi anaelekeza nani asajiliwe na
si kamati.
Hali hiyo ni tofauti na wenzao Yanga ambao
wameanza kufanya usajili wao kwa kuwanyakuwa Malimi Busungu kutoka
Mgambo JKT na Geofrey Mwashiuya kutoka Kemondo FC inayoshiriki Ligi
Daraja la Kwanza lakini kwa kufuata mapendekezo ya kocha Hans Pluijm.
Habari kutoka ndani ya Simba zinadai kuwa kocha
mkuu wa Simba, Goran Kopunovic tayari ametoa mapendekezo yake ya usajili
kwa viongozi juu ya wachezaji anaowahitaji kwenye msimu ujao kuwa
anataka kipa, beki wa kati, straika wa kati, winga na beki wa kulia.
Mchakato wa usajili ndani ya Simba umeanza ambapo
hadithi za kuwarejesha kundini maveterani wao Juma Kaseja na
mshambuliaji Mussa Hassan ‘Mgosi’ anayekipiga Mtibwa Sugar imeanza upya
huku kukiwepo na mabishano kati ya pande mbili za uongozi, wengine
wakiafiki wengine wakiwapinga maveterani hao.
Kwa sasa katika nafasi hizo zilizopendekezwa,
Simba inawategemea makipa wake wanne ambapo wawili ni kutoka U-20,
Manyika Peter na Denis Richard, Hussein Sharrif ‘Casillas’ na Ivo
Mapunda.
Casillas amedaka mechi moja tu ya Ligi Kuu dhidi
ya Polisi Moro ambayo walitoka sare ya bao 1-1 na baada ya hapo aliumia
ugoko wakati wa maandalizi ya mechi yao na Yanga ya raundi ya kwanza.
Ivo mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu
huku kukiwepo na taarifa za kutomwongeza mkataba mpya japokuwa awali
viongozi wa Simba walitangaza kutaka kumwongeza.
Nafasi ya beki wa kati kwa sasa wapo nahodha
Hassan Isihaka na Juuko Murshid pamoja na Joseph Owino anayemaliza
mkataba wake, straika akiwa ni Dan Sserunkuma na Elius Maguli, winga
anatumiwa Ramadhan Singano ‘Messi’ wakati beki wa kulia Hassan Kessy
ndiye anayetumainiwa kwa sasa ukiachana na William Lucian ‘Gallas’.
Ukiachana na Kaseja na Mgosi, mapendekezo mengine
yaliyopo kwenye meza ya Kamati ya Utendaji ni straika Ramadhan
Kiparamoto anayeichezea Abajalo FC, Masele Boniventure kutoka Majimaji
na wengine watatu wanaotarajiwa kupandishwa kutoka U-20.
Wachezaji wawili kutoka U-20 waliondoka na timu
juzi Jumatano kwenda Shinyanga kucheza na Kagera Sugar huku mmoja
akigoma kwa madai kuwa mpaka alipwe fedha zake anazodai.
Post a Comment