Yanga haikamatiki



Mashabiki wa Yanga wakishangilia kwenye Mechi yao na Mbeya City iliyochezeka jana kwenye Uwanja wa Taifa. 
AFRIKA Mashariki jana kulikuwa na mechi mbili kubwa kwenye Ligi za ndani, Kenya
kulikuwa na mpambano wa Mashemeji baina ya Gor Mahia na AFC Leopards ambao uliisha kwa sare ya bao 1-1. Lakini kimbembe kilikuwa Bongo, Yanga ilizidisha kiburi na jeuri kwa kuthibitisha kwamba msimu huu haikamatiki kotekote baada ya kuifumua Mbeya City mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga imeendeleza jeuri hiyo ikiwa ni siku chache baada ya kuinyuka Coastal Union mabao 8-0 huku ikiwa na kumbukumbu nzuri kimataifa baada ya kuipiga chini Platinum ya Zimbabwe na sasa inapiga kifua ikimaanisha Etoile du Sahel waje hata sasa hivi.
Vinara hao wa Ligi Kuu wamebakiza pointi tano tu kukata tiketi ya kucheza michuano ya CAF mwakani na pointi 11 kuwavua Azam ubingwa baada ya ushindi wao wa jana.
Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi 46, nane zaidi ya ilizonazo Azam yenye pointi 38 baada ya juzi kung’ang’aniwa tena na sare dhidi ya Mtibwa Sugar ikiwa ni mara ya pili mfululizo.
Pointi hizo zinaifanya Yanga kubakisha pointi tano ili kupata moja ya nafasi mbili za uwakilishi wa Tanzania katika michuano ya kimataifa na kuwafungia njia Simba wenye pointi 35 na inayoweza kufikisha pointi 50 tu ikishinda mechi zake zote.
Pia Yanga imebakiza pointi 11 tu kuweza kuwavua Azam ubingwa kwani itafikisha pointi 57 ambazo haziwezi kufikiwa na watetezi hao hata wakishinda mechi zao zote kwani itaweza kufikisha pointi 56 tu.
Katika pambano hilo lililochezeshwa vema na mwamuzi Mathew Akram, Yanga ilianza kwa kasi dakika tano za kwanza kwa kulishambulia lango la wapinzani wao na dakika ya sita Amissi Tambwe aliandika bao, lakini lilikataliwa kwani kabla ya kufunga mwamuzi wa pembeni alinyoosha kibendera.
Hata hivyo walisahihisha makosa katika dakika ya 18 baada ya Kpah Sherman kufunga bao la kwanza akimalizia shuti lililotemwa la Haruna Niyonzima. Hilo likiwa bao la pili kwa Mliberia huyo msimu huu.
Vijana wa Hans vand der Pluijm waliendelea kuliandama lango la wapinzani wao na kufanikiwa kuandika bao la pili katika dakika ya 37 kupitia kwa Salum Telela aliyefunga kwa shuti kali baada ya kuanzishwa mpira wa adhabu na Niyonzima.
Mbeya City waliotoka kuwabana Azam kwa kutoka nao sare ya 1-1 Jumatano iliyopita ilicharuka na kupata bao lao dakika tano kabla ya mapumziko kupitia kwa Themi Felix ‘Mnyama’ baada ya kuwafunga tela mabeki wa Yanga kabla ya kupiga ‘chop’ iliyoshindwa kudakwa na kipa Ali Mustafa.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Mbeya City kukosa mabao ya wazi kabla ya kuruhusu bao katika dakika ya 49 baada ya nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kuunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu ya Niyonzima. Mbeya ilipata pigo dakika nne baadaye baada ya Themi kulimwa kadi nyekundu na mwamuzi Mathew Akrama baada ya kumchezea madhambi Salum Telela. Telela alijikuta akishindwa kuendelea na mchezo huo na kutolewa nje na nafasi yake kuchukuliwa na Hassan Dilunga. Licha ya kucheza pungufu, Mbeya City waliibana Yanga na hasa baada ya kufanya mabadiliko ya wachezaji kwa kuwatoa Deus Kaseke, Raphael Alpha na Paul Nonga na kuwaingiza Peter Michael, Mwegane Yeya na Abdallah Seif.
YANGA: Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Mbuyi Twite, Salum Telela/Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Kpah Sherman/Mrisho Ngassa na Simon Msuva.

No comments