Simba yafanya kweli, Ukawa watoa msimamo. Hii ni habari kamili
SIMBA imezidi kuongeza presha kwa Azam baada ya jana kupata
ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar katika pambano la kiporo
uliochezwa kwenye uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Ushindi huo umeifanya Simba kupunguza pengo la
pointi baina yake na Azam kutoka nne hadi kuwa moja, kwani imefikisha
pointi 35 baada ya mechi 21, wakati watetezi hao wa Ligi Kuu wanaoshuka
uwanjani kesho kucheza na Mbeya City wana pointi 36 kutokana na mechi
18.
Mabao ya Simba katika mechi hiyo ya jana iliyokuwa
imelazwa toka Jumamosi kutokana na mvua yaliwekwa kimiani kupitia kwa
Ramadhani ‘Messi’ Singano aliyefunga kwa shuti kali dakika ya 49 kabla
ya Rashid Mandawa kusawazisha bao dakika ya 60 akimalizia krosi ya Adam
Kingwande.
Bao hilo limemfanya Mandawa kumkamata Didier Kavumbagu wa Azam katika ufungaji akiwa na bao 10.
Hata hivyo Simba ilijihakikishia ushindi katika
dakika ya 65 baada ya kupata penalti baada ya mabeki wa Kagera kuunawa
mpira na Ibrahim Ajibu kutumbukiza kiufundi mkwaju huo na kusaidia timu
yake kupata pointi tatu muhimu na kuwazima Kagera waliotamba kabla ya
mchezo huo.
SIMBA UKAWA
Mashabiki wa Tawi la Mpira na Maendeleo maarufu
Simba Ukawa, wamesema kuwa kundi lao kamwe haliwezi kufa kutokana na
vifo vya wenzao vilivyotokea Ijumaa kwa ajali ya gari kwani lina zaidi
ya wanachama 100 wenye uwezo mkubwa wa kuendeleza kundi hilo.
Katika ajili hiyo ya barabarani iliyotokea eneo la
Makunganya, Morogoro, ilisababisha vifo vya wanachama saba wa tawi hilo
akiwemo katibu wao Mohamed Kingolile ‘Ngumi Jiwe’ na jana Jumatatu
walimazia kumzika mwanachama wao Rashid Baltazar aliyezikwa Yombo Dovya,
Dar es Salaam.
Mweka Hazina ambaye pia ni mratibu wa safari za
Ukawa, Jaffari Mussa, aliliambia Mwanaspoti kuwa msiba waliopata ni
mkubwa ila hauwezi kuwazuia kuishangilia Simba katika mechi zao zozote
na hawawezi kuvunja kundi hilo.
Mratibu huyo pia alikemea vitendo vya baadhi ya
mashabiki wa Simba aliodai wanaeneza sumu kwa viongozi kuwa vitendo
hivyo haviisaidii Simba kimaendeleo na vinaleta migogoro.
“Tumepatwa na msiba huu viongozi wa Simba wamekuja
waliwakilishwa na Makamu wa Rais, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ aliyekuja
mpaka Morogoro hospitali, lakini kuna wanaojichanganya na sisi walitaka
kumfanyia fujo kwa kumfukuza, huo si utu wala uungwana.
Majeruhi watano kati ya 24 waliojeruhiwa katika
ajali hiyo watalazimika kuchunguzwa zaidi afya zao na madaktari bingwa.
Mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa mkoa wa Morogoro, Dk Ritha Lyamuya
alithibitisha hilo.
Post a Comment