Waarabu waishtukia Yanga, Simba watia mkono Dar
Etoile ambao ni wadeni wa Simba, watacheza na Yanga kwenye raundi ya pili ya michuano ya Kombe Shirikisho baada ya kuiondoa Benfica de Luanda ya Angola kwa mabao 2-1
YANGA ikishinda mechi nne zijazo kwenye Kombe la Shirikisho
itanukia utajiri, lakini Kocha wa Etoile de Sahel, Faouzi Benzarti na
mkurugenzi wake wa michezo, Zied Jaziri wameshtukia ishu kwamba wanaweza
kuumbuka wasipojipanga.
Etoile ambao ni wadeni wa Simba, watacheza na
Yanga kwenye raundi ya pili ya michuano ya Kombe Shirikisho baada ya
kuiondoa Benfica de Luanda ya Angola kwa mabao 2-1.
Yanga ambayo itacheza mechi ya kwanza Aprili 18
kwenye Uwanja wa Taifa itarudiana ugenini wiki mbili baadaye kisha
ikivuka itachezwa droo kwa kuchanganya na timu zilizotolewa kwenye
raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa ambapo zitachezwa mechi mbili kusaka
wa kuingia hatua ya makundi ya Shirikisho ambako ndiko kwenye mkwanja.
Vigogo wa Etoile wameonyesha kushtushwa na ufanisi
wa timu hiyo haswa kwa kuangalia kasi ya Yanga na kwamba wameamua
kujipanga upya kila idara tayari kwa lolote linaloweza kutokea huku
wakisisitiza kwamba wanaanza mashindano na Yanga.
Yanga ikifanikiwa kushinda mechi nne zilizosalia
na kutinga hatua ya makundi hata wakienda kuchemsha huko wana uhakika wa
noti kwani timu itakayokuwa ya mwisho kabisa kwenye kundi ina uhakika
wa Sh 270milioni pamoja na kuuza wachezaji wake, lakini ikikomaa ikiwa
angalau ya tatu itapata Sh432milioni.
Jaziri alisema jana kwamba licha ya joto kali na
changamoto walizokumbana nazo Angola wamevuka kutokana na kujituma na
juhudi za timu.
“Tunahitaji kuiangalia zaidi mechi ijayo (dhidi ya
Yanga) kwavile ndiyo itakayoamua mbio za ubingwa kwenye haya
mashindano,”alisema Jaziri.
Kocha Benzarti kwa upande wake alisema hakuna
mechi rahisi kwenye michuano hiyo ya Afrika ndio maana walijitahidi
kupata bao la mapema ili kumaliza mchezo dhidi ya Benfica na sasa
wameelekeza nguvu kwenye mechi na Yanga ili kuhakikisha wanarejesha
hadhi ya klabu hiyo.
Makamu wa Rais wa Etoile, Dr. Jalel Krifa alisema:
“Tumetimiza lengo moja kwa kuingia kwenye hatua nyingine muhimu bila
kuwa na majeruhi, tutapambana kwa jitihada zaidi katika mchezo unaofuata
kwavile ni muhimu zaidi kuliko huku tulikotoka.” Kiongozi huyo
aliongeza pia kwamba wana mzigo mkubwa kwenye mechi za Ligi Kuu ya
Tunisia hivyo wanahitaji kujipanga.
SIMBA WATIA MKONO
Simba inaidai Etoile du Sahel ya Tunisia Dola
300,000 zaidi ya Sh 500 milioni ikiwa ni deni la fedha za mshambuliaji
wao Emmanuel Okwi alipouzwa kwenye klabu hiyo ambapo viongozi wa klabu
hiyo wamesema watajadili jinsi ya kulipwa fedha hizo.
Mwishoni mwa mwaka jana, Shirikisho la Soka la
Kimataifa (Fifa) liliitaka Etoile kuilipa Simba fedha hizo baada ya
Simba kuishitaki kwa kushindwa kuwalipa kwa muda waliokubaliana lakini
mpaka sasa Watunisia hao hawajafanya lolote kwa Simba.
Next
Next
Post a Comment