REKODI: Bado mabao 23 Ronaldo avunje rekodi ya bernabeu




Mabao yake matano ya juzi dhidi ya Granada katika ushindi mnono wa mabao 9-1 wa Real yamefanya afikishe mabao 300 na hivyo kubakisha mabao 23 kumfikia mkongwe Raul Gonzalez ambaye anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi klabuni hapo akiwa na mabao 323 katika mechi 741

HISTORIA inakaribia kubadilika Santiago Bernabeu. Ni mshikemshike. Cristiano Ronaldo anaisaka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote Real Madrid na sasa amebakiza mabao 23.
Mabao yake matano ya juzi dhidi ya Granada katika ushindi mnono wa mabao 9-1 wa Real yamefanya afikishe mabao 300 na hivyo kubakisha mabao 23 kumfikia mkongwe Raul Gonzalez ambaye anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi klabuni hapo akiwa na mabao 323 katika mechi 741.
Ronaldo pia amebakisha mabao manane tu kufikia rekodi ya mkongwe anayeheshimika zaidi klabuni hapo marehemu, Alfredo di Stefano ambaye alifunga mabao 308 katika mechi 396.
Hata hivyo, inaonekana Ronaldo anaweza kuvunja rekodi zao akiwa amecheza mechi chache zaidi ambapo mpaka sasa ameichezea Real Madrid mechi 287 tu na kuna kila dalili msimu huu tu anaweza kuvunja rekodi hizo.
Mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa, Karim Benzema alikiri baada ya pambano hilo dhidi ya Granada kwamba Ronaldo alikuwa katika kiwango cha hali ya juu.
“Ronaldo ni mtu wa ajabu sana. siku zote anatafuta mabao na jinsi ya kuisaidia timu. Anastahili kila alichopata katika maisha yake ya soka,” alisema Benzema ambaye katika pambano hilo alifunga mabao mawili.
“Ronaldo, Bale na mimi tupo katika fomu nzuri, kama ilivyo siku zote. Tunaisaidia timu na wakati mwingine tunafunga na wakati mwingine hatufungi, lakini tupo katika hali nzuri na tutaendelea kuwa hivyo mpaka mwishoni mwa msimu,” aliongeza Mfaransa huyo.
Kwa upande wa Ronaldo mwenyewe, aliwapongeza wachezaji wenzake kwa kumsaidia kufunga mabao hayo matano wakati huu akiikaribia rekodi ya Raul ambaye aliondoka klabuni hapo mwaka 2010 baada ya kuichezea timu hiyo tangu mwaka 1994.
“Nafurahi nimefunga mabao matano kutokana na kazi nzuri ya timu. Asanteni kwa sapoti yenu,” aliandika Ronaldo katika mtandao wake binafsi wa mawasiliano wa Twitter.
Ushindi huo wa Real Madrid ulikuwa muhimu baada ya kupoteza mechi tatu kati ya tano za mwisho za La Liga ikiwemo pambano dhidi ya watani wao wa jadi katika soka la Hispania Barcelona walilochapwa 2-1.
Hata hivyo, ushindi huo uliiwezesha Madrid kukaa kileleni kwa muda tu baada ya juzi usiku, Barcelona kuichapa Celta Vigo bao 1-0 ambalo liliiwezesha kuendelea kuongoza La Liga kwa tofauti ya pointi

No comments