Kaseja sasa aibuka upya



KIPA wa zamani na nahodha wa Simba na Taifa Stars Juma Kaseja, juzi aliwashtua tena wapenzi na mashabiki wa klabu hiyo baada ya kuibuka kwenye mazoezi ya Simba yaliyofanyika Uwanja wa Chuo Kikuu, Dar es Salaam.
Ilikuwa hivi; Simba walianza programu zao uwanjani hapo mida ya saa tisa kama utaratibu wao wa kawaida chini ya Kocha Goran Kopunovic na Meneja wa timu hiyo Nico Nyagawa.
Ilipofika saa kumi kasoro, Kaseja aliwasili uwanjani hapo na kuzua maswali na mshangao kutoka kwa mashabiki na wapenzi wa timu hiyo waliojitokeza kwa wingi kwenye eneo hilo, kutazama mazoezi ya mwisho kwa Simba kabla ya kuelekea mkoani Shinyanga inapokwenda kukwaana na Kagera Sugar Jumamosi.
Minong’ono ilianza na wengi walihisi ujio wa Kaseja eneo lile, ni dalili za kipa huyo kurejea kwenye klabu yao aliyoidakia kwa mafanikio tangu mwaka 2003 akitokea timu ya Moro United.
Hata hivyo Mwanaspoti lilithibitisha kuwa Kaseja hakwenda kwenye uwanja huo kwa ajili ya Simba bali ujio wake pale ulitokana na uwepo wa mechi ya kirafiki kati ya wafanyakazi wa Chuo kikuu na timu ya makocha waliohitimu kozi ya daraja la pili ya ukocha iliyofanyika kwa muda wa wiki mbili na kufungwa juzi.
“Nimekuja hapa kwa ajili ya mechi yetu makocha dhidi ya wafanyakazi wa chuo si kwa ajili ya Simba. Imetokea tu tumekutana na Simba ambao wanafanya mazoezi hapa. Hakuna kikubwa zaidi ya hilo,” Kaseja aliithibitishia Mwanaspoti.
Katika mechi hiyo, timu ya Kaseja iliibuka na ushindi wa bao 1-0, lililofungwa na Twalha Musa huku kikosi chao kikijaza nyota wengi wa zamani kama Ally Mayay, Kassimu Mwabuda, Nico Nyagawa na Yahaya Issah.
Hii ni mara ya pili kwa Kaseja kuonekana katika mazoezi ya timu hiyo na kuibua hisia kwamba huenda akarudi.

No comments