Simba yaikomoa yanga
Straika wa Yanga Amissi Tambwe (aliyevaa jezi nyekundu) akiitumikia timu yake ya zamani, Simba SC
UAMUZI wa Yanga kumsainisha straika, Amissi Tambwe unaiumiza
Simba na uongozi umekiri kwamba Danny Serrunkuma wa Uganda bado
hajaonyesha walichokipandia ndege na kumfuata Kenya kumnunua.
Habari za ndani zinadai kwamba Simba ambayo safu
yake ya ushambuliaji bado haina mtu wa kati wa kuaminika, imekata tamaa
ya kumrudisha Tambwe baada ya Yanga kumuahidi mkataba wa maana hivyo
sasa ili kukata ngebe za wapinzani wao Mnyama ameamua kuingia msituni.
Kwahiyo? Simba wameanza mchakato rasmi wa
kitaalamu kusaka straika atakayeikomoa Yanga uwanjani kwa vitendo na
kuwasahaulisha mashabiki wa Msimbazi wasimkumbuke Tambwe. Uongozi pia
umeridhika na kiwango cha kocha wao, Goran Kopunovic. Rais wa Simba,
Evans Aveva ameitumia Mwanaspoti kuweka wazi kwamba Sserunkuma mwenye
mabao matatu bado hajafanya walichokitarajia katika usajili wake ingawa
hawajakata tamaa kwa kuwa anaendelea kuzoea mazingira ya Ligi Kuu
Tanzania Bara.
Alisema wanajua kwamba Kopunovic anataka straika
wa kati mwenye kujua kufunga ambapo tayari wameanza mchakato wa siri
kusaka kifaa na pia wanaendelea kufuatilia uwezo wa mshambuliaji wao
Raphael Kiongera ambaye kwasasa yupo Kenya kwa mkopo.
“Hata sisi tunaona hilo pengo la timu yetu kukosa
mshambuliaji wa kati, lakini nikwambie tu watu husika kwa kazi ya
kutafuta wachezaji wameanza kazi ya kutafuta mshambuliaji mkali mwenye
uwezo mkubwa wa kufunga lakini pia tunamfuatilia Kiongera kwa kuwa bado
ni mali yetu,”alisema Aveva.
“Kwasasa tunaye Sserunkuma (Danny) lakini tunakiri
kwamba bado hajafanikiwa kutupa kile tulichokitarajia kutoka kwake
katika hilo hatujakata tamaa soka ni mchezo wa subira kidogo tunaendelea
kumpa muda kwa kuwa ligi bado atazoea tu.”
Akizungumzia majaliwa ya Kopunovic ambaye mkataba
wake wa miezi sita wake unamalizika mwisho wa msimu huu, Aveva alisema
kwasasa uongozi wake unaimani kubwa na kocha huyo baada ya kuitoa timu
hiyo kutoka nafasi ya nane mpaka sasa ipo katika nafasi ya nne.
Alisema bado hajajua nini kitafanyika mwishoni mwa msimu ambapo kwasasa wanasubiri ripoti ya kamati ya ufundi.
“Tunafurahia kazi ya Kopunovic katika timu yetu
tuseme ule ukweli ukiangalia aliikuta timu yetu katika nafasi ya nane
ambayo haikuwa nafasi nzuri kulingana na ukubwa wa timu yetu na sasa
tupo nafasi ya nne na tunaendelea kupambana.”
“Tunaendelea kumpa ushirikiano kwa kila
analohitaji tunasubiri mambo mazuri zaidi katika mechi zilizosalia
lakini kuhusu nini tutaamua mwisho wa msimu tunasubiri kwanza ripoti ya
kamati ya ufundi baada ya ligi kumalizika.”
Post a Comment