Hawa jamaa hatari kwa magoli ya vichwa





TEKERO inadaiwa lilikuwa ni jina la mganga mmoja maarufu wa zamani aliyewahi kutamba katika moja ya mikoa ya Tanzania. Jina hilo alikuja kupewa mmoja wa mastraika mahiri kuwahi kutokea nchini, Abeid Mziba.
Nyota huyo wa zamani kutoka Kigoma aliyetamba na timu kadhaa kabla ya kutua Yanga. Aliichezea Taifa Stars kwa takriban miaka 10. Alikuwa mkali aisee. Mkali wa mabao ya kichwa. Wapo waliokuwa wakiamini alichanjia kichwa na kumfanya apigapo mpira ulikuwa ukienda kwa kasi kama umepigwa kwa miguu.
Siyo kama hakuwahi kufunga mabao kwa miguu. Alikuwa akifunga ila kwa nadra mno, kama lile la mwaka 1987 kwenye Uwanja wa Majimaji alipoipa Yanga ubingwa wa Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu).
Mwenyewe aliwahi kudokeza kuwa, alibashiriwa kufunga bao hilo la mguu wa kulia na kuizamisha Majimaji, lakini ni baada ya kukosa mabao mengi ya wazi. Ilidaiwa siku hiyo alikuwa amebeba nyota ya jaa ya Yanga katika mchezo huo wa Songea.
Kichwa chake kilithibitisha kuwa ni fundi wa mipira ya vichwa. Kipindi akiwa kwenye chati ndipo kukaibuka viatu aina ya raba vilivyotengenezwa na vitambaa vilivyopapatikiwa sana. Achana na HD, kuna maalumu vilivyopewa jina la Mziba kwa sababu mwenyewe alipenda kuvivaa enzi hizo.
Wapo pia waliovuka mipaka na kutania eti miguu ya Mziba ilikuwa ni ya kutembelea tu na siyo ya kuchezea soka. Ingawa ukweli ni kwamba alikuwa akifunga na kutoa pasi zilizozaa mabao kwa miguu hiyo hiyo iliyobezwa.
Sasa kama ulikuwa ukidhani baada ya kuondoka Mziba katika ulimwengu wa soka la uwanjani, ndiyo ingekuwa mwisho wa kuibuka kwa wakali wengine wa mabao ya vichwa umekosea.
Orodha ya wakali wa mabao ya vichwa waliomfuata Mziba ni ndefu, ikiwajumuisha kina Hamis Gaga ‘Gagarino’, Said Mwamba ‘Kizota’, Said Mrisho ‘Zico wa Kilosa’, Kitwana Manara ‘Popat’ na wengineo.
Hata hivyo, hapa chini tumewataja baadhi ya wachezaji walionyesha umahiri wao wa kufunga mabao ya aina hiyo.
SAMATTA
Nyota huyo anayekipiga TP Mazembe, anatajwa kama mmoja wa mafundi wa mipira ya vichwa. Samatta aliyeanza kufahamika African Lyon kabla ya kupita Simba kwa muda na kutimka zake kula maisha yake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, amekuwa akifunga mabao mengi kwa vichwa kuliko miguu yake, ingawa hata huko nako ni hatari.
Mfano mdogo ni katika msimu wa 2011-2012 wa Ligi ya Mabingwa Afrika, akiwa na kikosi hicho cha TP Mazembe kilichovutiwa naye baada ya kung’ara na Simba msimu mmoja nyuma yake, alicheza mechi nane.

No comments