Adui wa Simba aanikwa live...
KOCHA Mkuu wa Simba amewatahadharisha wachezaji na viongozi wa Simba kwamba mechi yao ijayo dhidi ya Kagera Sugar ni kama vita kwani wakiteleza tu wameumia.
Goran Kopunovic alisema Kagera Sugar ndiyo adui wao mkubwa kwa sasa katika harakati zao za kumaliza pazuri katika Ligi Kuu.
Kopunovic raia wa Serbia alisema katika mazoezi
yao yaliyoanza jana kuwa wanataka kujifua kwa nguvu kuhakikisha
wanakwenda kuchukua pointi tatu dhidi ya timu hiyo watakayoumana nayo
Jumamosi ijayo.
Alisema Kagera ndiyo adui wao mpya kutokana na
kuwa chini yao katika msimamo wa Ligi Kuu kwani kama itapoteza mechi
hiyo inaweza kuwa hatari kwao katika mbio za kuelekea juu.
Alisema katika kuyakimbia mazingira hayo anataka
kutumia wiki moja kuwaandaa wachezaji wake kupambana katika Uwanja wa
Kambarage Shinyanga ambao ulishawapa mazingira magumu kwa kufungwa na
Stand United ya huko kwa bao 1-0.
“Kwa sasa Kagera ni adui katika safari yetu,
tukifanya makosa tunaweza kuwa hatarini katika mbio zetu, nataka kuona
Simba inashinda ndiyo maana nataka timu ianze mapema mazoezi,” alisema.
“Ukiangalia msimamo utagundua tumewazidi mchezo mmoja, hatujui nini
kitatokea katika mechi hiyo, endapo watashinda wanaweza kutukaribia
zaidi. Kuwakimbia ni lazima tushinde, naujua sasa uwanja wao wa
Shinyanga, najua nilipoteza pale lakini sasa najua cha kuifanya.” Katika
hatua nyingine, Simba inakabiliwa na mchezo mgumu wa ugenini dhidi ya
Kagera ikiwa hatarini kuwakosa nyota wake watatu. Nyota hao ni kipa Ivo
Mapunda, beki Joseph Owino na winga Ramadhani Singano ‘Messi’ walio
majeruhi. Hata hivyo, cha kufurahisha ni kwamba, beki wao Juuko Murshid
aliyekuwa akiiwakilisha nchi yake ya Uganda katika pambano lao na
Nigeria na kuibuka washindi wa bao 1-0, amerejea. wakati Emmanuel Okwi
ana ruhusa maalumu kwenda kwao, lakini inadaiwa ataiwahi mechi na
Kagera.
Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alianika hayo
jana: “Ivo, Singano na Owino ni majeruhi na Okwi yupo kwao Uganda na
Murshid tunatarajia kumpokea akitoka kuwakilisha nchi yake,” alisema
Manara.
Alidokeza timu itaondoka mapema wiki ijayo kuwahi
pambano hilo. Katika hatua nyingine, kundi la wanachama wa Simba
linakwenda Zanzibar kwa ajili ya Michezo ya Pasaka wakiwa wageni wa
Kikwajuni.
Post a Comment