Simba yagundua uchawi wa Msuva
WAKATI Simba wakiweweseka na kasi ya mabao aliyonayo Simon Msuva wa Yanga, kinara huyo wa mabao wa Ligi Kuu ni kama amewafichulia siri yake.
Msuva mwenye mabao 11, matano kati ya hayo
akiyafunga kwa kichwa, mawili kwa penalti na manne kwa mguu alifichua
kuwa wala si uchawi kama watu wanavyofikiria bali ni ujanja wake wa
kuiba muda wa kocha wake, Mholanzi Hans Pluijm wanapokuwa mazoezi ili
kujifunza kufunga ndiyo sababu ya kumfunika Didier Kavumbagu mwenye
mabao 10.
Aliweka wazi kuwa, amekuwa akiwasumbua, Juma Abdul
na Mnyarwanda Mbuyu Twite mara kwa mara wampigie mipira ya krosi na
yeye amalizie kufunga kwa kichwa au mguu huku makipa, Deogratius Munishi
‘Dida’ na Ally Mustapha ‘Barthez’ akiwaomba wakae golini.
Alisema, amekuwa akifanya hivyo karibu kila
kipindi cha mazoezi na kila mmoja amekuwa anamwomba ampigie mipira
mitano au sita na kwa upande wa makipa mbali na kuokoa mipira hiyo ya
krosi, huwa anawapigia mipira mingine mitano ya penalti kila mmoja.
Akizungumza na Mwanaspoti, Msuva alisema:
“Ninatamani kufunga, napenda nifunge na hamu yangu ni kufunga lakini
pale ninapoweza faida ya klabu na mimi mwenyewe, nikawa nafanya sana
mazoezi ili nifanikiwe.”
“Nimekuwa nikiwasumbua sana baadhi ya wachezaji
mazoezini, huwa naibia mwalimu anapokuwa amesimamisha programu yake kwa
muda mfupi, huwa nawaomba wanipigie krosi na mimi nijaribu kufunga kwa
kichwa na miguu makipa wakiwa golini. Wakati mwingine nawaomba pia
wachezaji wa katikati wanichezeshee mipira nayo nafunga ni hivyo tu,”
alisema Msuva ambaye amefunga mabao ya kichwa katika mechi waliyocheza
na Prisons mzunguko wa kwanza bao moja, raundi ya pili mawili dhidi ya
Prisons, moja na Mbeya City na moja dhidi ya Azam.
“Lakini pamoja na hamu yangu hiyo, huwa
silazimishi kufanya hivyo, ninapokuwa sina uwezo, pia namwomba Mungu
anilinde na majeraha ili nitimize malengo yangu ya kufunga kadri
niwezavyo ili niwe mfungaji bora na timu yangu ichukue ubingwa.”
Msuva ambaye kuna habari kwamba Simba inamuwania
pia aling’ara kwa mabao kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi ambalo
hata hivyo ni mahasimu wao Simba ndio waliobeba taji la michuano hiyo.
REKODI
Awali Msuva alikuwa anacheza straika wa kati
katika klabu mbalimbali alizopitia kama, Azam FC, Moro United na timu za
Taifa za vijana chini ya miaka 17 na 20.
Baada ya kutua Yanga, alihamishiwa pembeni nafasi
ya winga na yeye anasema: “Sina tatizo kucheza nafasi hiyo, kama una
uwezo wa kufunga mabao, kokote utafunga iwe straika wa kati au winga
pembeni.”
Kocha wake mkuu, Mholanzi Hans Pluijm amesifu kiwango cha Msuva kuwa ni mchezaji anayefuata maelekezo na kukubalia mabadiliko.
Post a Comment