Simba hatarini kumpoteza straika huyu machachari
SIMBA inaweza kumpoteza mshambuliaji wake Mkenya, Raphael
Kiongera, baada ya kushindwa kumlipa mshahara wake wa mwezi Desemba na
Januari na amesema kwamba anasubiri wafikishe miezi mitatu ili achukue
uamuzi mgumu.
Kiongera ambaye kwa sasa anafanya mazoezi na timu
yake ya zamani KCB na ataichezea kwa mkopo wa miezi mitano, aliliambia
Mwanaspoti kuwa mkataba wake upo wazi kwamba asipolipwa mshahara miezi
mitatu, basi mkataba huo utakuwa umevunjwa.
Alisema ni mara nyingi amekuwa akiwapigia simu
viongozi wake juu ya kuwakumbusha mishahara yake lakini wamekuwa wakimpa
ahadi zisizotekelezeka.
“Unajua kwa sasa siwapigii simu tena, nimechoka
kuzungushwa ila ninachokifanya ni kusubiri miezi mitatu ipite ili
nichukue uamuzi wangu kwani watakuwa wamevunja mkataba wenyewe, haya ni
maisha na mimi nategemea kuishi kupitia mpira, sasa wasiponilipa
mshahara wanategemea naishije?” alihoji.
“Tulikubaliana kuanza kuichezea Simba msimu ujao
ingawa daktari aliniambia naweza kuanza kucheza mwezi huu, wao
walimsajili mchezaji mwingine lakini leo hii wanashindwa kunilipa
mshahara wangu, wanataka niwabembeleze, ngoja nione mwisho wake ni
nini.”
Kiongera alifanyiwa upasuaji wa goti mwaka jana
nchini India na Simba ndio waliotoa gharama zote za matibabu kwa
mshambuliaji huo, kwa kutumia Sh15 milioni.
Usajili wake Simba ulikuwa ni wa Dola 20 (Sh34
milioni) kwa miaka miwili na ameichezea Simba mechi moja tu ya ufunguzi
dhidi ya Coastal Union waliyotoka sare ya bao 2-2.
Kwa mujibu wa makubaliano ya pande zote mbili,
Kiongera ataanza kuichezea Simba msimu ujao wa ligi na sasa atacheza kwa
mkopo KCB kulinda kipaji chake.
Imeelezwa beki Joseph Owino ndiye atakayetemwa
katika usajili wa msimu ujao na nafasi yake itachukuliwa na Kiongera.
Owino atakuwa amemaliza mkataba wake.
Hata hivyo, viongozi wa Simba walipoulizwa juu ya suala la straika huyo, hawakutoa ushirikiano.
Post a Comment