Yanga ni kimataifa zaidi.. Hawa ndio watakaoivaa BDF XI ya Botswana Jumapili
WAWAKILISHI wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho, Yanga, wamewafunika vibaya wapinzani wao katika michuano hiyo, BDF XI ya Botswana katika takwimu.
Kwa kuangalia takwimu hizo ni wazi kwamba miamba
hiyo ya Jangwani inaweza kufanikiwa kuwaondosha DBF na kusonga mbele
kwenye michuano hiyo.
Rekodi za BDF kwenye ligi ya Botswana msimu huu
zinaonyesha timu hiyo inashika nafasi ya tatu na pointi 37 wakiwa
wamecheza mechi 19 wakati Yanga wao wanaongoza Ligi Kuu Bara wakiwa na
pointi 25 baada ya kucheza mechi 13.
BDF wamefungwa mabao 20 msimu huu ikiwa ni wastani
wa bao moja katika kila mechi jambo linaloashiria kuwa wanafungika
kirahisi wakati Yanga wao wamefungwa mabao saba pekee ikiwa ni wastani
wa bao moja kwa mechi mbili jambo linaloleta matumaini ya ushindi kwa
Yanga.
Yanga pia imepoteza mechi mbili pekee msimu huu
wakati BDF wao wamefungwa mechi sita. Mabingwa hao wa mwaka 2013
wameonekana kuwa kwenye fomu zaidi wakiwa hawajapoteza mchezo wowote
katika mechi sita za mwisho kwa kushinda mechi nne kati ya sita za
mwisho za ligi na kutoka sare mbili wakati DBF wao wamefungwa mechi moja
na kushinda tano katika mechi zake sita za mwisho.
Kocha wa Yanga, Hans Van Plujim alisema mechi hiyo
ya kimataifa ni ngumu kwa Yanga lakini ushindi walioupata juzi Jumapili
dhidi ya Mtibwa umepandisha morali yao na kuwapa nafasi kubwa ya
kuibuka na ushindi.
“Unapokwenda kucheza mechi kubwa kama hiyo ya BDF
na timu yako imetoka kushinda ni jambo zuri, morali ya wachezaji inakuwa
juu na kila mtu anakuwa na ari ya ushindi, haitakuwa kazi rahisi
lakini,” alisema.
“Bado hatujapata nafasi ya kuwaona wapinzani wetu,
lakini tutafanya maandalizi ya kutosha kwa muda wa wiki nzima ili
kujiweka pazuri, ni lazima tushinde mchezo huo wa kwanza na kuwaondoa
katika mchezo wa pili ili tuweze kusonga mbele.”
Yanga itakuwa mwenyeji wa BDF Jumapili.
Post a Comment