Kopunovic akataa kuitoa Simba
KOCHA Mkuu wa Simba, Goran Kopunovic, amepanga kesho Jumatano
kikosi chake kitangulie mkoani Morogoro kuwafuata Polisi ya huko lakini
ametamka kwamba kama kuna anayedhani Simba imejiondoa katika mbio za
kuwania taji la Ligi Kuu Bara huyo anajidanganya.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kopunovic alisema
amepata taarifa kwamba baadhi ya mashabiki wameiondoa Simba katika mbio
za ubingwa ambapo ametamka kwamba ni makosa makubwa kufikiria hilo.
Alisema kutokana na msimamo wa Ligi pamoja na
mechi zilizosalia, bado Simba ina nafasi ya kugombea nafasi mbili za juu
kwani mazingira wanayokutana nayo bado Yanga na Azam waliopo juu
wanaweza kukutana nayo.
Alisema bado ana imani na kikosi chake na kwa sasa
wanataka kusaka ushindi kwa staili ya kuangalia mechi zao huku
wakisubiri wanaoongoza ligi kukumbana na mazingira magumu katika mechi
zao.
“Mimi naangalia mambo kwa tofauti na wanavyofanya
wengine, angalia mechi zilizosalia kwa timu zote utagundua kwamba yoyote
anaweza kufanya makosa kama ambavyo Simba tumefanya,” alisema
Kopunovic.
“Siku zote naiandaa Simba kushinda lakini kupata
sare haya ni matokeo ya mpira, mazingira kama haya yanaweza kuzikumba
timu zozote zilizopo juu yetu, tunachofanya sasa ni kujiandaa kwa mechi
zetu tukisubiri kuona nini kitatokea kwa wapinzani wetu.”
Post a Comment