Mrwanda anywa maji ya kishirikina



MASTRAIKA wawili wa Yanga wamekumbana na uchawi wa aina yake. Kpah Sherman ambaye ni Mliberia amedai kuyabaini maji ya ushirikina yaliyokuwa uwanjani, lakini mwenzake Danny Mrwanda akayachukua akayanywa huku kipa aliyeyaweka akiwashangaa.
Kpah ambaye si mzungumzaji sana, alifichua tukio hilo lililotokea kwenye mechi yao ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Ndanda kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo timu hizo hazikufungana.
Lakini mlinda mlango wa Ndanda, Wilbert Mweta, ambaye ni kipa wa zamani wa Simba, aliposikia maneno ya Sherman akashangaa. Katika mchezo huo, washambuliaji wa Yanga; Sherman, Mrwanda na Simon Msuva walikosa mabao ya wazi wakiwa peke yao mbele ya lango, kila walipopiga mipira ilipaa na kutoka nje hali ambayo iliwashangaza wapenzi wa soka na mashabiki waliofika uwanjani hapo. Hata hivyo kocha wa Yanga, Hans Pluijm, amepuuza madai hayo na kusema ni uzembe tu wa wachezaji wake.
Sherman ameiambia Mwanaspoti kwamba kwenye goli la Ndanda kulikuwa na maji ya ushirikina na aliyatoa kwa mikono yake baada ya kugundua kwamba kipa huyo aliyanyunyizia kwenye goli na baadaye akayabakiza mengine na kuyaweka pembeni ya mlingoti wa lango.
Baada ya Mliberia huyo kuyatoa maji hayo na kuyatupa nje, bado yalikuwa magumu kwao kisha Mrwanda aliyafuata na kuyanywa. Hata hivyo haikusaidia chochote kwani ndio kwanza wapinzani wao walizidi kukaba huku wakijiangusha kupoteza muda.
Sherman aliiambia Mwanaspoti akisema: “Mimi ni Mwafrika moja kwa moja naamini maji yale yaliwekwa vitu tu vya kishirikina ikawa sababu ya kutukosesha mabao, ndiyo maana niliamua kuyatupa nje, haiwezekani mtu na goli unapaisha.
“Pia nilimwona kwa macho yangu yule kipa, yale maji aliyamimina (anaonyesha kwa ishara) kuanzia mwanzo wa goli hadi mwishoni kwa nini alifanya vile ndio yalikuwa kikwazo kwetu,”alisema Sherman ambaye Yanga wanamchukulia kuwa ndiye straika namba moja wa timu yao.
Ingawa Mrwanda hakupenda kufafanua hilo, kipa Mweta alijitetea akisema: “Ule ni mpira ndiyo maana tunafanya mazoezi, hakuna ushirikina wala nini.
“Nimeshangaa sana kuona mchezaji mkubwa kama yule kuamini mambo hayo ya kishirikina badala ya kucheza mpira, anajua kiwango chake ni kidogo?”
Kocha Pluijm alisema hawezi kuwalaumu washambuliaji wake kutokana na kitendo cha kushindwa kufunga mabao na badala yake anaulaumu mfumo wa makuzi ya soka waliyokulia wachezaji hao tangu utoto wao.
Pluijm alisema suala la kufunga ndiyo jambo kubwa alilokuwa akiwaelekeza katika kipindi chote cha mazoezi yao na walikuwa wanafanya vizuri mazoezi. Alisema aligundua tatizo hilo katika michezo waliyocheza na Polisi Morogoro na Ruvu Shooting.
“Hatufungi, sina wasiwasi na safu ya ulinzi lakini kwa washambuliaji tatizo lao ni ufungaji, nimekuwa nikilifanyia kazi kwa siku zote kwenye mazoezi yetu na wachezaji walikuwa wanafanya vizuri,” alisema kocha huyo.

No comments