Yanga yaonyesha jeuri ya pesa




KLABU ya Yanga kupitia Mwenyekiti wake, Yusuf Manji imewasilisha pendekezo mbele ya marais wanaounda Umoja wa Afrika (AU) la kuanzisha mashindano maalumu ya kupambana na ugonjwa wa Ebola na akatoa Dola 500,000 (sawa na Sh 870 milioni) kwa kuanzia.
Fedha hiyo aliyotoa Manji inakaribiana na fedha anayopewa bingwa wa Kombe la Shirikisho, mashindano ambayo Yanga inashiriki mwaka huu ikianza na BDF XI ya Botswana Jijini Dar es Salaam.
Bingwa wa Shirikisho hupewa Dola 625,000 (Zaidi ya Sh1 bilioni) huku mshindi wa pili akipata Dola 432,000 (Sh700 milioni za Tanzania).
Yanga imetenga Sh160 milioni kwa ajili ya mechi mbili dhidi ya BDF ambayo ni bajeti tofauti kabisa na hiyo ya Ebola aliyotoa Manji.
Pendekezo hilo la Manji amelitoa Alhamisi ya Januari 29 wiki iliyopita jijini Addis Ababa, Ethiopia kulikofanyika mkutano huo ambao kwa nchi ya Tanzania uliwakilishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete huku Manji akiwa mmoja wa wageni.
Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu wa Yanga, Dk. Jonas Tibohora, ambaye naye aliongozana na Manji alisema katika kikao hicho cha 24 cha AU, Manji amewasilisha pendekezo hilo akitaka nchi 54 za Afrika kushiriki katika mashindano hayo mafupi kusaka fedha za kupambana na ugonjwa huo hatari unaiosumbua Afrika Magharibi. Katika mapendekezo ya Manji anapendekeza watakaoshiriki mashindano hayo wawe mabingwa wawili wa juu wa kila nchi.
Tibohora alisema katika pendekezo hilo la Manji ambalo nchi zote zililiafiki, Manji ametaka mashindano hayo kuchezwa kwa kanda za nchi husika ambapo mechi hizo zitachezwa kwa mfumo wa nyumbani na ugenini huku kila klabu ikitakiwa kuchangia kiasi cha dola 100,000 (Sh173 milioni ) kama kiingilio.
Alisema lengo la Manji ni kutaka kuona soka linachangia katika mapambano ya ugonjwa huo ambapo jumla ya kiasi cha dola 10.8 milioni zitaweza kupatikana huku Mwenyekiti huyo akitangulia kutoa hizo dola 500,000 za kianzio.
“Kwa kuwa mechi hizo zitakuwa zikiendeshwa kwa mfumo wa nyumbani na ugenini, Manji ameomba klabu itakayocheza nyumbani itoe nusu ya mapato ya kwenye mechi husika iende katika mapambano hayo hapo pia klabu zitanufaika na nusu ya mapato hayo lakini pia ushindani huo utazinufaisha baadhi ya nchi.”
KATUMBI KUFURU
TAJIRI wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Moise Katumbi, amekuwa na aina ya kipekee ya uendeshaji wa timu yake kwa kuwapa zawadi watu wanaompa furaha uwanjani kwa wakati wote.
Habari kutoka kwenye vyanzo vya kuaminika hapa Lubumbashi zinaeleza kuwa mchezaji anayefunga bao moja katika mechi za kimataifa hupewa zawadi ya dola 10,000 (Sh 18 milioni) na anayetoa pasi ya bao hilo hupewa zawadi ya dola 5,000 (Sh 9 milioni)

No comments