Sserunkuma athibitisha
KWA kipindi kirefu mashabiki wa Simba walianza kupoteza imani na mshambuliaji wao Mganda Dan Sserunkuma kutokana na kushindwa kwake kuzifumania nyavu.
Baadhi ya mashabiki na hata wanachama wa Simba
katika kutapatapa na matatizo yaliyokuwa yakiikabili timu yao, walianza
kumnyooshea kidole mshambuliaji huyo na kumuona si mwenye msaada katika
timu.
Fikra na mtazamo huo umekuja kutokana na imani
kubwa waliyokuwa nayo mashabiki hao kwa mshambuliaji huyo ambaye alikuwa
moto wa kuotea mbali wakati akiichezea Gor Mahia ya Kenya.
Kwa kuwa akiwa na Gor Mahia aliibuka Mfungaji Bora
wa Ligi Kuu Kenya, baadhi ya mashabiki waliamini kasi hiyo ya mabao
ingeendelea katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara na kwamba mshambuliaji huyo
angeanza moja kwa moja kwa kufunga.
Baada ya kuona matarajio yao hayatimii wakaanza
kupoteza imani naye na kujenga hisia kwamba klabu yao imesajili mchezaji
mzigo na wengine kuja na dhana kwamba hajitumi na hivyo Simba haihitaji
kuendelea kuwa naye.
Matokeo mabaya ya kufungwa na Mbeya City mabao 2-1
ndiyo yaliyoongeza hasira za mashabiki wa Simba na katika kusaka
mchawi, Sserunkuma naye akaingizwa katika kundi hilo hilo la wachezaji
wasio na msaada Simba.
Hata hivyo wapo japo wachache waliojenga imani
kwamba mshambuliaji huyo alihitaji muda wa kuzoea mambo mengi yakiwamo
mazingira na hata uchezaji wa timu kwa ujumla.
Na pengine imani hiyo ya wachache imeanza
kuthibitika katika mechi ya juzi ya Ligi Kuu Bara ambako Simba iliibuka
na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya JKT Ruvu, mechi iliyopigwa kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kilichoanza kumkuta Sserunkuma kinatukumbusha mambo ya kukatishana tamaa katika soka la Tanzania.
Cha kufurahisha ni kwamba uongozi wa Simba hakukuwa tayari kumezwa na hisia za kwamba Sserunkuma ni mzigo.
Uvumilivu ambao umeonyeshwa na viongozi hasa
makocha wake ndilo jambo ambalo linatakiwa kufuatwa na viongozi na hata
mashabiki wa klabu nyingine. Ni kweli kwamba kila shabiki wa Simba
alipenda kumuona mchezaji huyo akiendeleza kasi yake upachikaji mabao
kama ilivyokuwa wakati akiwa nchini Uganda.
Na hata timu pinzani kwa kuzingatia rekodi ya mchezaji huyo pengine waliamini kwamba angekuwa na madhara makubwa kwa timu zao.
Post a Comment