Mastaa hawa wanatarajia kung’oka Simba
SHABAN Kisiga amelitumia Mwanaspoti kuwaeleza mashabiki zaidi ya
milioni 20 wa Simba ukweli wake wa rohoni wa nini hasa kinachoendelea
na kilichomtoa kwenye timu hiyo.
Hata hivyo, alichosisitiza zaidi ni kwamba ilikuwa
inamdhalilisha kwa kumkalisha benchi ila Mwanaspoti limepata habari za
uhakika kutoka ndani kwamba kuna wachezaji wawili wakongwe nao
watamfuata kiungo huyo.
Wachezaji hao ni kipa Ivo Mapunda (pichani) ambaye
ndiye mchezaji pekee wa Simba aliyewahi kuwa askari akaacha kazi na
beki Nasoro Masoud ‘Chollo’ ambao hata hivyo mikataba yao itamalizika
mwishoni mwa msimu, huku Awadh Juma, Elius Maguri na Jonas Mkude
wanadaiwa kuwa na nidhamu mbovu na wanachunguzwa kimya kimya.
Kisiga ambaye anaishi Yombo jijini Dar es Salaam,
aliliambia Mwanaspoti kuwa alikuwa akivumilia hali hiyo kwa kuamini
kwamba mambo yangebadilika, lakini haikuwa hivyo hata pale alipokuja
kocha mpya Mserbia Goran Kopunovic ambaye aliendelea kumwingiza akianzia
benchi.
Alisema anaamini kama Kopunovic (48), angekuwa ameachwa huru kupanga kikosi huenda angekuwa anapewa nafasi ya kucheza.
“Niliamua kuondoka kwa sababu niliona nadhalilika
sana na kwa nini nifikie hatua hiyo? Mimi si mchezaji wa kupewa dakika
10 au tano kucheza, inaumiza sana hasa pale unapojua ni kwa nini
hupangwi, yote haya yalikuwa yanatokea kwa chuki ya mtu jambo ambalo
mimi huwa sikubaliani nalo,” alisema Kisiga ambaye amewahi kuichezea SC
Villa ya Uganda.
“Hivyo ni vyema niondoke ili niwaachie wengine
ambao wana nafasi ya kucheza kuliko kwenda kambini unakula na kulala
bure halafu huchezi, najua hawaumii juu yangu kwani hata usajili wangu
ni wa kawaida sana ukilinganisha na wachezaji wao waliowasajili kwa
mamilioni ya fedha, lakini mimi nazingatia heshima yangu.”
Kiungo huyo mtaalamu wa kupiga faulo, alisema kuwa
inasikitisha kuona mpira wa Tanzania kwa sasa unaendeshwa kwa fitina na
si kuzingatia uwezo wa mchezaji husika ukoje.
“Najua hata kocha alipotua tu Zanzibar aliambiwa
watu wa kuanza kuwapanga na wale wa kuanzia benchi, hizo ni fitina mbaya
ambazo zinaua viwango vya wachezaji wengi hapa nchini, mpira hautaki
majungu, uwezo wa mtu unaonekana uwanjani.
“Mwaka jana nilisimamishwa pamoja na wenzangu
wawili (Amri Kiemba na Haruna Chanongo), nilirudishwa nikapewa unahodha
msaidizi huku jukumu kubwa likiwa kusimamia wachezaji vijana ambao mimi
ni wadogo zangu, sasa kwa nini thamani yangu haionekani kwa ajili ya mtu
mmoja? Staa anaonekana kwa ubora si kwa kubebwa.”
Akifafanua juu ya uhusiano wake na Kocha Msaidizi,
Selemani Matola, alisema: “Sina ugomvi na Matola ila ni kiongozi ambaye
ana majungu, huenda aliacha mpira wakati maisha yake yakiwa hayajakaa
vizuri hivyo akiona mwenzake anafanikiwa roho inamuuma, lakini maisha
hayaendi hivyo.”
Hata hivyo, Matola ambaye ni nahodha wa zamani
mwenye jina kubwa Simba, alisema jana kuwa yeye hana ugomvi wowote na
Kisiga na wala hakuwahi kugombana naye siku za nyuma.
Post a Comment