Twite amtokea kocha wa Yanga usiku wa manane
MHOLANZI pekee kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara anayeinoa Yanga,
Hans Pluijm (66), ameushangaa uamuzi wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) kugoma kusogeza mbele mchezo wao dhidi ya Mtibwa wa Machi 8,
lakini akasimulia maajabu mazito yanayomtokea akiwa usingizini kuhusu
kiraka wake, Mbuyu Twite.
Pluijm ametamka kwamba katika hali isiyo ya
kawaida, kuna wakati akiwa amelala usiku mnene inamjia sauti ikimwarifu
kwamba beki huyo ni msaada mkubwa kwenye timu.
Alisema sauti hiyo imekuwa ikimtokea wakati beki
huyo akiwa majeruhi na mara moja imewahi kumtokea akiwa na Yanga Misri
wakati wakijiandaa kucheza na Al Ahly ya Misri msimu uliopita kwenye
Ligi ya Mabingwa Afrika walipotolewa kwa penalti.
Alisema pia usiku wa kabla ya mchezo wa juzi
Jumatano dhidi ya Coastal Union mjini Tanga, aliisikia tena sauti hiyo
na alipoamka siku ya mchezo akakuta mchezaji huyo yupo fiti na
alipompanga akafanya kazi kubwa ya kuwazuia washambuliaji wa Coastal
huku mpira wake wa kurusha ukizaa bao pekee lililoipa ushindi Yanga
likifungwa na nahodha, Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
“Sijui ni nini, lakini hayo ndiyo huwa yananitokea
na nikija uwanjani utaona kweli Twite anakufanyia kazi yako vizuri, ni
mpambanaji mzuri ambaye siku zote amekuwa hataki kufanya makosa,”
alisema Pluijm ambaye alioa Oktoba 6, 1971.
“Nidhamu yake ya uwanjani haina tofauti kubwa na
ile ya nje ya uwanja, hana tofauti kubwa na Cannavaro (Nadir Haroub)
ambaye naye amekuwa mfano mzuri wa mabeki sio wa Yanga pekee hata wa
timu nyingine,” aliongeza kocha huyo ambaye timu yake ilipoifunga
Coastal shabiki maarufu wa Yanga, Ally Yanga, alipigwa jiwe katika paji
ya uso na kupoteza fahamu. Ally ambaye hupenda kuvaa kitambi huku uso
wake akipaka vumbi la mkaa alikutana na kasheshe hilo katika Uwanja wa
Mkwakwani wakati akishangilia bao la Cannavaro na shabiki mmoja wa
Coastal alimrushia jiwe hilo ambalo lilimpoteza fahamu kabla ya
kuwahishwa hospitali.
Kichekesho ni pale ambapo Ally alirudiwa na fahamu na kutoroka hospitali alipoambiwa na muuguzi kwamba Yanga imeshinda.
“Viatu sijui viko wapi mimi nimetoroka pale
hospitali, nilishangaa kujikuta nipo hospitali lakini nikauliza swali
moja matokeo ya Yanga vipi, mhudumu akaniambia kwamba Yanga imeshinda
bao lilelile moja akinitaka nitulie alipotoka nikasema hapa hapa
naondoka,” alisimulia Ally huku waliokuwa karibu yake wakiangua vicheko.
Post a Comment