Zengwe jingine laibuka ndani ya Yanga..
YANGA imeibua zengwe jipya ambalo huenda
likaidhohofisha timu ya Polisi Morogoro ambayo usajili wake wote
hauzidi Sh40 milioni. Pesa hizo ni thamani ya straika mmoja wa Yanga,
Kpah Sherman.
Polisi Morogoro, ambayo
haijawahi kushinda mchezo tangu straika wake, Danny Mrwanda aende Yanga,
inacheza na Yanga mjini Morogoro kesho Jumamosi kwenye mechi ya Ligi
Kuu na Yanga imeamua kuiibulia zengwe ambalo huenda likatibua mipango
yao kama litafanikiwa.
Yanga imesisitiza kwamba straika
Said Bahanuzi iliyemtoa kwa mkopo Polisi Morogoro haruhusiwi kucheza
dhidi yao Jumamosi na akichezeshwa wanalianzisha. Bahanuzi ndiye straika
aliyefunga bao moja na pekee la Polisi kwenye mechi tatu mfululizo.
Polisi baada ya kuondokewa na Mrwanda imecheza mechi tatu, ikasuluhu
mbili dhidi ya Stand na Coastal pamoja na sare ya bao 1-1 na Ndanda.
Lakini Polisi wamesisitiza
kwamba ni lazima Bahanuzi acheze kwani walikubaliana kuhusu jambo hilo
tangu anasaini. Katibu wa Polisi, Leus Yazidi, aliliambia Mwanaspoti
kuwa walikubaliana na Yanga wamtumie katika mechi zote za Ligi Kuu hata
dhidi yao hadi atakapomaliza mkopo wake wa miezi sita katika klabu hiyo
inayomilikiwa na Jeshi la Polisi.
“Unauliza kuhusu Bahanuzi?
Ndiyo, tutamtumia katika mechi yetu na Yanga kwani ni moja kati ya vitu
tulivyokubaliana wakati tunamsajili kwa mkopo kutoka kwao. Tutamtumia,
na sasa tunamuandaa ili atupatie ushindi dhidi ya timu yake ya zamani,”
alisema Yazidi.
Wakati Polisi ikiamini hivyo,
Katibu wa Yanga, Jonas Tibohora alisema Polisi haiwezi kumtumia
Bahanuzi katika mchezo dhidi yao kwani kanuni zilizopo ni kwamba
mchezaji anayecheza kwa mkopo timu nyingine haruhusiwi kucheza dhidi ya
timu yake labda kuwe na makubaliano maalumu ya maandishi.
“Bahanuzi hawezi kucheza dhidi
yetu, ndivyo kanuni zinavyosema sasa kama wao wanasema watamtumia sawa
tutaona nani mshindi katika kanuni, wala hatuna tatizo,” alisema
Tibohora ingawa kwenye kanuni za uhamisho wa wachezaji wa Ligi Kuu Bara
hakuna kipengele kinachosema mchezaji asicheze dhidi ya timu
iliyomkopesha.
Kwa upande wake, Bahanuzi
alisema amejipanga vilivyo kuwatoa nishai mabeki wa Yanga, Nadir Haroub
‘Cannavaro’, Kelvin Yondani na Mbuyu Twite kwani anawajia kivingine na
wajiandae.
“Nipo kazini sitajali kwamba
Yanga nimeitumikia miaka miwili nitakachoangalia ni jinsi gani
nazitikisa nyavu zao naomba tu ushirikiano kutoka kwa wachezaji wenzangu
kwani mabeki wao nawajua jinsi walivyo, nimejifunza mbinu mpya tangu
nilipotua Polisi Moro nikiongeza na za kwangu naamini nitaisumbua safu
ya ulinzi ya Yanga, nimejipanga naomba uzima kwa siku hiyo,”alisisitiza
mchezaji huyo, ambaye haogopi zengwe la Yanga.
Post a Comment