Sserunkuma ni moto kwa sasa
STRAIKA wa Simba, Elius Maguli amesema
ameshafahamu aina ya uchezaji wa straika mwenzake, Danny Sserunkuma na
wakiendelea kucheza pamoja wanaweza kufunga mabao zaidi.
Maguli na Sserunkuma wote
waliifungia Simba ilipoilaza Ndanda mabao 2-0 wikiendi iliyopita na
kufufua matumaini ya safu ya ushambuliaji ya timu hiyo iliyoshindwa
kufunga mabao mengi katika michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyomalizika
punde huko visiwani Zanzibar.
Maguli alisema awali alipata
tabu kufahamu aina ya uchezaji ya Sserunkuma lakini kwa kadiri siku
zinavyozidi kwenda wamekuwa wakizoeana na huenda wakafanya makubwa zaidi
siku zijazo.
“Nashukuru kwa sasa tumeanza
kufanya vizuri, kama unavyojua Danny (Sserunkuma) alikuja wakati timu
imebadili kocha, haikuwa kazi rahisi kwa kocha mpya kujua namna ya
kutuchezesha kwa pamoja.
“Tumeendelea kufanya kazi katika
mazoezi ya timu kuhakikisha tunazidi kuelewana ili tuweze kufunga
zaidi, siyo kazi rahisi lakini tunapambana,” alisema Maguli, ambaye
alifunga mabao 14 akiwa Ruvu Shooting msimu uliopita.
“Mwanzoni pia kufunga ilikuwa
kazi ngumu kwasababu timu ilikuwa haifanyi vizuri, ile hali ilitusumbua
sana kwani morali ya timu ilishuka na kila wakati tukawa tunajihisi
wanyonge.”
Wakati huohuo, katika mazoezi ya
Simba juzi Jumanne jioni kwenye Uwanja wa Boko Veterani, Sserunkuma
alishindwa kutamba kwenye zoezi la ufungaji baada ya mashuti yake sita
aliyopiga kushindwa kulenga goli na mengine kuokolewa na makipa
akimwacha, Emmanuel Okwi raia wa Uganda aking’ara.
Pamoja na hayo, Kocha wa Simba,
Goran Kopunovic alisema: “Kiujumla sina wasiwasi kabisa na kiwango cha
Sserunkuma katika timu yangu.
Namwamini na ndiyo maana
nimekuwa namtumia kila wakati. Sserunkuma ni mchezaji mzuri sijui hapo
awali, lakini sasa kadri ya siku zinavyozidi ubora wake umekuwa
unaongezeka, anajiamini na kufanya maamuzi sahihi, nafikiri hapo awali,
woga na ugeni ndivyo vilivyokuwa vinamsumbua,”alisema Kopunovic.
Simba inajiandaa na mechi yao ya ligi watakayocheza keshokutwa Jumamosi katika Uwanja wa Taifa dhidi ya Azam FC.
Post a Comment