Yanga yatoa onyo kwa TFF kuhusu haya...



HAPA kazi ipo. Yanga imevumilia na kuamua kutoa onyo kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juu ya vitendo vya kibabe wanavyofanyiwa wachezaji wake katika mechi zake.
Timu kubwa za soka nchini, Simba, Yanga na sasa Azam FC, zimekuwa zikikumbana na vitendo vya kibabe na udhalilishaji kwa nyota wake hasa wanapocheza na timu nyingine za Ligi Kuu bara na kukaa kimya.
Lakini Yanga imeamua kuweka wazi kukerwa na tabia hizo baada ya wachezaji wake akiwemo straika Amissi Tambwe kuchezewa kibabe na mabeki wa Ruvu Shooting wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa.
Tambwe amesimulia mateso anayoyapata kutoka kwa mabeki wa timu pinzani katika mechi za ligi hiyo na kuwataja wawili ambao ni vinara kwa kazi hiyo kila anapokutana nao uwanjani.
Lakini wakati Tambwe akilalamikia undava anaochezewa, mojawapo ya timu alizokumbana nazo, Ruvu Shooting imeibuka na kusema: “Hana lolote ameshindwa kuhimili muziki wetu.”
Akizungumza na Mwanaspoti Tambwe ambaye ni raia wa Burundi alisema katika maisha yake ya soka nchini amekuwa akikutana na mateso makubwa kutoka kwa mabeki watatu ambao wamekuwa wakimfanyia vitendo visivyofaa vinavyoambatana na udhalilishaji.
Tambwe alisema beki wa kwanza katika kazi hiyo ni George Osei ambaye amekuwa akimfanyia vitendo hivyo ikiwemo kumkaba vibaya katika kila mchezo. Osei sasa anachezea Ruvu Shooting ambayo wikiendi iliyopita ilitoka suluhu na Yanga.
Alisema mabeki wengine ni Sunza Shaaban maarufu kwa jina la Chogo ambaye sasa anachezea Mwadui ya Shinyanga, lakini alikuwa anakumbana naye wakati anacheza Ruvu pia, wa mwisho ni Michael Aidan wa timu hiyo hiyo.
“Hao mabeki wamekuwa wakinitesa sana, sina maana kwamba sitaki kukabwa lakini ni wazi hawastahili kucheza soka kwa njia wanazofanya, hawanitendei haki hata kidogo. Hawa wanakukaba huku wakikuambia maneno mbalimbali yasiyofaa mara wewe mkimbizi, hivi wanajua vita kweli hawa? Mimi naijua vita wasithubutu kumwambia mtu mkimbizi,” alisema Tambwe.
“Kuna huyu Aidan nimeambiwa na wenzangu aliwahi kuitwa hata timu ya taifa ya Tanzania lakini kuna mambo ambayo anayafanya ipo siku ataisababishia Tanzania madhara makubwa kama atachezeshwa, hawa wanatakiwa kufungiwa ili wajifunze.”
Awali Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro alisema uongozi wao umesikitishwa na matukio ya Tambwe kunyanyaswa na kupigwa uwanjani ambapo jana waliwasilisha malalamiko yao kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) huku wakiorodhesha mapendekezo yao matano.
Muro alisema wanaitaka TFF kuwachukulia hatua kali wahusika wote waliobainishwa kufanya vitendo hivyo huku wakitaka ripoti ya mchezo huo kuwekwa hadharani kubaini mapungufu ya waamuzi.

No comments