Yanga yamtenda vibaya Mrisho Ngassa
Kuendelea kukatwa makato makubwa imeelezwa ndiyo chanzo cha kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngassa, kudorora uwanjani.
Ngassa amekuwa kwenye kiwango cha chini msimu huu ikiwa ni tofauti na misimu mingine yote iliyotangulia.
Kiungo
huyo, alitua kuichezea timu hiyo kwenye msimu wa 2013/2014, kwa
makubaliano ya kulipa fedha shilingi milioni 45, ikiwa ni deni la
shilingi milioni 30 pamoja na faini ya milioni 15 za Simba ili aweze
kuitumikia timu yake ya Yanga.
Ngassa alitakiwa kulipa fedha hizo, baada ya kusaini mara mbili Simba na
Yanga na kama angeshindwa, basi angefungiwa kucheza soka na kulipishwa
faini kutokana na kitendo hicho.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka kwa rafiki wa karibu wa kiungo
huyo, Ngassa ameshindwa kucheza katika kiwango chake kutokana na
viongozi wa Yanga kumsusia deni la shilingi milioni 45 anazodaiwa na
Simba.
Chanzo hicho kilisema kwa makubaliano waliyokubaliana kila mwezi, kiungo
huyo alitakiwa kukatwa shilingi 500,000 katika sehemu ya mshahara wake,
lakini baadaye mambo yakabadilika akawa anakatwa shilingi 1,000,000.
“Wengi wanahoji kiwango cha Ngassa kimeshuka lakini hawajui sababu, hivi
sasa hayupo vizuri, amechanganyikiwa kisaikolojia kutokana na deni
analodaiwa kususiwa na Yanga, iliyoamua alipe mwenyewe badala ya klabu
kumsaidia kama walivyokubaliana alipotoka Simba.
“Katika makubaliano yao, yeye alitakiwa kukatwa kiasi cha shilingi
500,000 kwa kila mwezi na klabu imuongezee kiasi flani cha fedha
kitakachokwenda kwenye deni alilokopa ili ailipe Simba fedha zao
walizokuwa wanamdai.
“Kutokana na kiasi hicho cha fedha anachokatwa, anakosa kabisa fedha za
matumizi yeye na familia yake kwa kuwa anabakiza kiasi kidogo kwenye
mshahara wake.
“Isitoshe hizo fedha zenyewe anazokatwa hazionekani kuongezeka kwenye
akaunti hiyo iliyofunguliwa kwa ajili ya kulipia deni hilo la mkopo
anaodaiwa, hiyo ndiyo sababu ya msingi Ngassa anashindwa kucheza kwa
kujituma ikiwemo kufunga mabao.”
Alipotafutwa Ngassa kuzungumzia hilo alisema: “Hizo taarifa umezipata
wapi? Ni kweli kabisa hizo taarifa, kisaikolojia akili yangu haipo
vizuri kutokana na deni ninalodaiwa, ukiangalia kiasi cha fedha
ninachokatwa kwa kila mwezi ni kikubwa ambacho hatujakubaliana hivyo.
“Tulikubaliana kuwa klabu inisaidie kulipa deni la mkopo niliouchukua
ili niwalipe Simba kwa makubaliano ya mimi kukatwa 500,000 lakini
ninashangaa imekuwa tofauti, wananikata 1,000,000 katika mshahara wangu.
Post a Comment