Hawa ni Mastaa wanne wa Yanga wanaohujumiwa..
Kocha wa Yanga, Hans Pluijm akiwa katika pozi kwenye mazezi
KOCHA wa Yanga, Hans Pluijm, amegundua hujuma za kuwafanyia rafu
na kuwaumiza makusudi wachezaji wake wanne kwenye mechi za Ligi Kuu
Bara na ameahidi kupambana nazo ingawa amewaonya waamuzi kuwa makini.
“Yanga kila mchezo inaocheza ni kama fainali,
kunakuwa na vita kubwa kati ya wachezaji wangu na mabeki wa timu
pinzani, sitaki kusema nataka wasikabwe lakini kuna tatizo katika namna
ya kuwazuia wanaumizwa sana tena kwa makusudi kabisa,” alisema Pluijm.
“Timu yangu inaundwa na wachezaji wenye majina,
hakuna timu inayotaka kufungwa, lakini tatizo ni jinsi wanavyokabiliana
na wachezaji wangu. Marefa wawe makini zaidi katika kuangalia ni jinsi
gani wanakabwa, ili kuepuka madhara,”anasisita Pluijm.
Wachezaji hao wanne ambao Pluijm amesema
wanafanyiwa fujo na hujuma za waziwazi uwanjani huku waamuzi
wakishuhudia ni Amissi Tambwe, Kpah Sherman na viungo wa pembeni Andrey
Coutinho na Simon Msuva.
Ametamka kwamba wamekuwa wakiumizwa bila sababu za
msingi na mabeki wasio waungwana wa timu pinzani jambo ambalo limekuwa
likiathiri kasi ya Yanga ambao imesuka kikosi cha kutwaa kombe msimu
huu.
Pluijm amesisitiza kwamba hataki timu yake
ipendelewe na waamuzi, lakini akawaonya waamuzi hao kuhakikisha
wanaongeza umakini kugundua rafu wanazochezewa washambuliaji wao ambao
wamekuwa wakikamiwa vibaya na timu pinzani.
Katika hatua nyingine pia Mholanzi huyo
amesisitiza kwamba Deo Munishi ‘Dida’ ndiye kipa namba moja nchini,
lakini kinachomsikitisha wapo watu wanamkatisha tamaa badala ya kumpa
moyo anapokosea.
Dida alikosa mechi yao ya Jumamosi dhidi ya Ruvu
Shooting waliyotoa suluhu na Ally Mustapha ‘Bartez’ ndiye alidaka mchezo
huo. Yote ni kutokana na madai kuwa ameshuka kiwango na hakufanya
vizuri katika mechi zake za mwisho hasa walipocheza na Azam FC wakatoa
sare ya mabao 2-2.
Akizungumza na Mwanaspoti, Pluijm alisema:
“Napenda ushindi na mpira ni ushindi, lakini nakubali pia soka ni mchezo
wa makosa. Yapo makosa yanaweza kutokea kwa binadamu yoyote bila
kutegemea.”
“Mfano, binafsi naamini kuwa, Dida ni namba moja,
anayefanya vizuri kwenye soka la Tanzania, lakini kuna mambo
yanayofanyika kama kumkatisha tamaa jambo ambalo linaweza kumharibia,
akapotea kabisa mchezoni,”alisema Pluijm.
“Yapo makosa na yanatokea hata Ulaya ipo hivyo kwa
anayeangalia soka la huko anajua. Kama Dida alifanya makosa yanaweza
kumtokea binadamu yoyote na kinachotakiwa kufanya ni kumpa moyo ili awe
vizuri na arudi katika hali yake, lakini siyo kumkatisha tamaa, anaweza
kupotea kabisa.”
Post a Comment