Yanga ijifunze haya kutoka kwa Simba.




MASHABIKI wa Simba wamekuwa wakiwakejeli wenzao wa Yanga kwamba hawana jeuri ya kujiamini kumsimamisha langoni kipa chipukizi kama wao wanavyofanya kwa Manyika Peter na wachezaji wengine wa nafasi za ndani.
Wanadai kwamba Yanga hawana uvumilivu uliopo Simba ingawa wenzao wamekuwa wakicheka yanapoanza mabishano hayo kwenye Uwanja wa Taifa na vijiwe vinavyouzunguka uwanja huo siku ya mechi.
Lakini kipa huyo ameweka rekodi ya aina yake Msimbazi ndani ya mechi sita zilizopita na kuziacha solemba Yanga na Azam zenye makipa wazoefu. Manyika amecheza mechi sita chini ya kocha Mserbia Goran Kopunovic bila ya kuruhusu nyavu zake kutikiswa.
Safari hiyo ya Manyika aliianza katika Mashindano ya Kombe la Mapinduzi ambapo katika hatua ya makundi alicheza dakika 180 bila kuruhusu bao huku pia akiendeleza rekodi hiyo katika mechi za robo fainali, nusu fainali na fainali.
Kipa huyo alihamishia rekodi hiyo katika mechi ya Ligi Kuu ambapo katika mchezo wa jumamosi iliyopita alikuwa langoni kwa dakika 90 Simba ikishinda kwa mabao 2-0 na kumfanya kufikisha dakika 540 bila kufungwa.
Akimzungumzia kipa huyo Kapunovic alisema Manyika amekuwa na kazi nzuri ambayo inatokana na utulivu wake langoni pamoja na umakini wa mabeki wake, ingawa wanafanya makosa lakini wamekuwa wakijua jinsi ya kujipanga na kujisahihisha.
“Anafanya vizuri kwangu mimi ukiwa na umri kama huu wa Manyika na ukafanya kazi yako sawa ni jambo linalovutia, hili linatokana na umakini wa mabeki haina maana kwamba hawafanyi makosa, lakini inapotokea wanafanya makosa wanajua jinsi ya kujisahisha,”alisema Kopunovic.
Katika mechi sita za mwisho Kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’ amedaka zote na kuruhusu bao moja dhidi ya JKU kwenye Kombe la Mapinduzi. Lakini kabla ya kuingia kwenye Mapinduzi Deo Munishi ndiye aliyedaka timu hiyo ilipotoka sare ya mabao 2-2 na Azam.
Mtibwa nayo imo
Mtibwa imecheza mechi 15 za mashindano bila kupoteza. Mtibwa imecheza michezo tisa ya Ligi Kuu Bara bila kupoteza, ikishinda michezo minne na kutoka sare mingine mitano huku ikifunga mabao 12 na kufungwa matano pekee.
Mbali na hilo Mtibwa ilicheza michezo sita ya Kombe la Mapinduzi bila kupoteza mchezo wowote ndani ya dakika tisini kwani ilifungwa na Simba katika mechi ya fainali kwa mikwaju ya penalti baada ya mchezo kumalizika kwa suluhu.
Kwenye ligi Yanga wamecheza michezo tisa kama Mtibwa lakini imefungwa mechi mbili, ikatoka sare tatu na kushinda michezo minne.

No comments