MIKIKIMIKIKI ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon
2015) itaanza kutimua vumbi leo Jumamosi kwa wenyeji Guinea ya Ikweta
kukipiga na Congo kabla ya Burkina Faso kukwaruzana na Gabon.
Kesho Jumapili michuano hiyo itaendelea kwa
Mabingwa wa Afrika 2012, Zambia kushuka uwanjani kuchuana na DR Congo,
kabla ya Tunisia kucheza na Cape Verde.
Fainali hizo za 30 zitaanza kwa matumaini ya
mashabiki kupata uhondo na burudani bab’kubwa ya mchezo wa soka licha ya
kukumbwa na changamoto nyingi ikiwamo hofu ya maradhi ya Ebola.
Awali fainali hizo zilitarajiwa kufanyika Morocco,
lakini nchi hiyo ilijitoa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kupeleka
uwenyeji wa michuano hiyo katika nchi ya Equatorial Guinea.
Mechi za michuano hiyo zitafanyika katika miji
minne mikubwa, Bata, Malabo, Mongomo na Ebebiyin ambako viwanja vingi
vipya vilivyojengwa kwa ajili ya fainali hizo bado havijakamilika
vizuri, huku uwanja uliopo Ebebiyin umeripotiwa kuwa na uwezo wa
kuingiza mashabiki 5,000 tu.
Mwaka 2012 uwanja huo uliweka rekodi baada ya mashabiki 200 tu kwenda kutazama mechi hizo.
Kutokana na mwamko mdogo wa mashabiki kwenda
uwanjani kutazama mechi jambo hilo limemfanya rais wa nchi hiyo, Teodoro
Obiang Nguema kununua tiketi 40,000 kwa ajili ya kuzigawa kwa mashabiki
ili wajitokeze kwenye michezo hiyo.
Ebola yatishia usalama
Virusi vya maradhi ya ugonjwa huo vilianza
kusambaa maeneo ya Afrika Magharibi Machi, mwaka jana na kusababisha
vifo vya watu 8,386 katika nchi sita tofauti hadi kufikia Januari 12,
mwaka huu.
Uwepo wa maradhi hayo unatishia hali ya usalama wa
kiafya na jambo ambalo linaweza kutibua zaidi fainali hizo
zikashuhudiwa na mashabiki wachache.
Hata hivyo, kwa nchi ya Equatorial Guinea hakuna
mgonjwa wa Ebola iliyewahi kuripotiwa kutokea katika ardhi hiyo baada ya
kuajiri madaktari wataalamu wa kueneza elimu ya kuepuka maambukizi.
Kwenye ukanda huo wa Afrika Magharibi nchi
zilizoathirika zaidi ni Guinea, Sierra Leone na Liberia na kwamba
wachezaji wote wanaokwenda kwenye fainali hizo walifanyiwa vipimo kuona
kama kuna mwenye virusi hivyo vya maradhi hayo hatari. Timu inayopewa
nafasi ya kushinda taji ni Algeria.
Post a Comment