KATIKA hali isiyotarajiwa, mashabiki wa Yanga waliokuwa na dukuduku la moyoni, juzi Alhamisi jioni walimfuata Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Boniface Mkwasa na kumtaka abadilishe mpangilio ili badala ya kumtumia straika Mrundi, Amissi Tambwe kuwa straika wa pili, amchezeshe akiwa straika namba moja na Mliberia, Kpah Sherman, ndiye awe straika namba mbili.
“Samahani kocha kwanza pole na kazi, tulikuwa na
maoni kwamba Tambwe acheze namba tisa na Sherman acheze 10, maana
tuliona katika Kombe la Mapinduzi mlikuwa mnawabadilisha sasa tumeona
Tambwe anamudu sana tisa hapo tutapata mabao mengi,” alisema mmoja wa
mashabiki hao huku akiungwa mkono na wenzake waliomzunguka Mkwassa
kwenye Uwanja wa Boko Vetereni.
Katika kutoa ufafanuzi, Mkwasa aliwaambia kuwa
hivyo ndivyo walivyopanga kuwachezesha kwa kuwabadilisha ili kuwazoesha
wasikariri namba moja.
Jibu hili lilionekana kutowaridhisha mashabiki
hao, lakini walimshukuru kocha huyo na kisha kumwambia tangu wameanza
kukinoa kikosi hicho kimekuwa na mabadiliko makubwa na kinawapa
matumaini ya kufanya vema katika mechi za Ligi Kuu Bara na Kombe la
Shirikisho.
Katika hatua nyingine, beki wa Yanga ambaye pia ni
nahodha, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amemwambia kocha wa Simba, Goran
Kapunovic, kuwa kazi si kuchukua Kombe la Mapinduzi, bali kushinda
mechi za Ligi Kuu Bara.
“Tunaamini Yanga nzuri ingawa tulitolewa katika
Kombe la Mapinduzi, mechi zile si kipimo kwamba timu yake ni nzuri. Huku
kwenye ligi ndiyo sehemu ambayo Simba inatakiwa kuonyesha ubora
wake,”alisema Cannavaro.
“Nimeona watu wanampongeza sana huyu kocha mpya wa
Simba hata mimi nampongeza kwa ubingwa wa Mapinduzi, lakini ili watu
wajue ubora wake anatakiwa ashinde mechi za ligi.”
Post a Comment