Yaliyosemwa na madaktari baada ya Okwi kutoka hospitali..




MADAKTARI waliomhudumia straika wa Simba, Emmanuel Okwi baada ya kuumia kwenye mechi dhidi ya Azam juzi Jumapili,  wamethibitisha kwamba anaendelea freshi lakini mmoja wao akatikisa kichwa na kueleza kwamba kama wangezembea kumpa huduma ya kwanza ingekuwa hatari na pigo kubwa.
Daktari maalum wa Simba, Yassin Gembe amethibitisha kwamba mchezaji huyo amerudi kwenye kambi ya mazoezi ya Simba na anaendelea kuwa chini ya uangalizi wa kina.
 Hali ya Okwi raia wa Uganda imeimarika  baada ya kupatiwa matibabu katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Okwi alitolewa uwanjani dakika ya 61 katika mchezo huo wa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam akiwa hajitambui baada ya kugongana na mchezaji mwenzake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Gembe alisema: “Naweza kusema, Okwi alipata majeraha hatari ambayo yametishia maisha yake, kuzimia kupo kwa aina nyingi, lakini hii ya kwake ilikuwa hatari, ikatishia amani  kwa sababu pumzi ilikata kabisa.
“Lakini baada ya kupatiwa matibabu ya kina na kujiridhisha hali yake imeimarika na anaendelea vizuri na tupo naye kambini kwa ajili ya uangalizi zaidi.”
Alisema vipimo vyote vilikamilika saa 2:30 usiku wakaruhusiwa kurudi nyumbani.
Katibu Mkuu Chama cha Madaktari wa Michezo (Tasma), Nassor Matuzya alisema: “Inaonyesha alipoteza fahamu jambo ambalo huenda limesababishwa na ubongo kucheza, kitaalamu ni ‘Concussion’.
“Kutokana na tatizo lake kama asingepatiwa matibabu ya kina, huenda yangetokea mengine, kama siyo kifo, basi moja ya viungo vyake katika mwili kinachoenda na sehemu ya ubongo  iliyoumia kisingeweza kufanya kazi.”
Matuzya aliongeza kwamba  mpango wao sasa ni kufanya semina kwa madaktari wa timu na wanaohudumia uwanjani kujua namna ya kukabiliana na majeruhi mbalimbali.
Alisisitiza, kunapotokea tatizo kama hilo linapochelewa kupatiwa matibabu ndiyo ukubwa wa tatizo unaongezeka.
Awali daktari wa Tasma aliyemuhudumia Okwi uwanjani baada ya tukio hilo, Richard Yomba alisema: “Okwi alipoteza fahamu kwa muda na baada ya kupatiwa huduma ya kwanza alipata fahamu na kupelekwa Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.

No comments