Man City yamkodia ndege Yaya Toure kuivaa Chelsea
MAJI yapo shingoni na hakuna jinsi. Imebainika kuwa Manchester City imeandaa ndege maalumu ya kuwarudisha haraka England kiungo Yaya Toure na mshambuliaji Wilfried Bony kwa ajili ya pambano la Chelsea Jumapili kama Ivory Coast ikiondolewa katika michuano ya Afcon kesho Jumatano.
Kocha wa Manchester City, Manuel Pellegrini tayari
alikuwa amejiandaa kuwa bila ya Toure na Bony mpaka katikati ya Mwezi
Februari kutokana na wachezaji hao kuwepo nchini Guinea ya Ikweta
wakishiriki michuano ya Mataifa ya Afrika.
Lakini licha ya kuwa kileleni katika msimamo wa
Kundi D, Ivory Coast inaweza kutupwa nje ya michuano kama ikipoteza
dhidi ya Cameroon Jumatano na City ipo tayari kukodi ndege ya
kuwarudisha mastaa hao Manchester haraka kwa ajili ya safari ya London.
City imeshindwa kushinda mechi yoyote tangu
kuondoka kwa Toure, ikitoka sare na Everton, kabla ya kupoteza mechi
mbili mfululizo dhidi ya Arsenal na Middlesbrough katika uwanja wao wa
nyumbani Etihad.
Huku mshambuliaji wake mahiri, Sergio Aguero
akisumbuka kurudi katika fomu tangu atoke katika majereha ya goti mapema
mwezi huu, umuhimu wa uhamisho wa Bony umeanza kuonekana baada ya timu
hiyo kufunga bao moja tu katika michezo mitatu iliyopita.
Mara baada ya kuwasili kutoka katika mapumziko ya
siku tano nchini Abu Dhabi Ijumaa jioni, ikiwa ni saa 24 kabla ya
pambano la FA dhidi ya Middlesbrough, Pellegrini amedai kwamba
hawakupoteza pambano hilo kutokana na uchovu.
Lakini baada ya City kupoteza pointi tano mbele ya
Chelsea katika uongozi wa ligi huku ikichangiwa kwa kiasi kikubwa na
kukosekana kwa Toure, inadaiwa kuwa Toure na Bony watapelekwa Manchester
haraka kuwahi pambano la Stamford Bridge Jumamosi kama Ivory Coast
itatupwa nje ya michuano hiyo na Cameron.
Endapo jambo hilo litatokea, kumbukumbu zitarudi
nyuma karibu miaka mitano iliyopita wakati mshambuliaji wa zamani wa
City, Carlos Tevez aliporudishwa Manchester haraka kutoka kwao Argentina
saa chache kabla ya mechi ya Chelsea jijini London.
Tevez alifanikiwa kushirikiana vizuri na Craig
Bellamy na kuihenyesha Chelsea na kushinda mabao 4-2 ugenini na hicho
kuwa kipigo cha kwanza Chelsea katika ligi msimu huo.
Post a Comment