Wachezaji hawa ni tishio kwa mkwanja msimu ujao..


UTAKE usitake, winga Simon Msuva wa Yanga yupo katika ubora wa juu kwa sasa. Amefanikiwa kupandisha thamani yake uwanjani ndani ya muda mfupi.
Licha ya makosa yake madogo madogo na ubinafsi uwanjani, bado Msuva anabaki kuwa moja ya nguzo muhimu katika kikosi  cha Yanga. Hakuna mtu mwenye wasiwasi na uwezo wake.
Licha ya ubora wake huo, Msuva hawezi kupiga pesa yoyote pale Yanga kwa sasa. Alisaini mkataba mpya kabla ya kuanza kwa msimu na atalazimika kusubiri kwa mwaka mmoja zaidi ili aweze kupata mkataba mpya. Maisha hayajamtendea haki. Yanga pia haina mpango wa kumuuza kwenda timu nyingine.
Ukiachana na Msuva, wapo mastaa kadhaa ambao wamefanikiwa kupandisha thamani zao na wanatarajiwa kupiga pesa za maana mwishoni mwa msimu. Mwanaspoti inakuletea orodha ya mastaa hao;

Didier Kavumbagu, Azam FC
Straika Mrundi, Didier Kavumbagu anajiamini na anaamini katika kile anachokifanya uwanjani. Kavumbagu alijiunga na Azam mwanzoni mwa msimu huu baada ya kumaliza mkataba wake na Yanga. Licha ya kuachwa Yanga baada ya mkataba wake, Kavumbagu alisaini mkataba wa mwaka mmoja pekee pale Azam na hakuwa na papara ya kutaka mkataba wa muda mrefu. Aliamini katika kazi yake na kile anachokwenda kukifanya uwanjani. Wachezaji wengi wanaogopa mikataba hiyo mifupi kwa hofu ya kushuka viwango na kutemwa mwisho wa msimu lakini kwa Kavumbagu ni tofauti. Tayari ameifungia Azam mabao saba katika mechi 10 za Ligi Kuu Bara na kuiwezesha timu hiyo kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi na pointi 20. Kwa sasa straika huyo anasubiri msimu umalizike apige pesa za maana katika mkataba mpya.

Ame Ally, Mtibwa
Straika wa Mtibwa Sugar, Ame Ally ni miongoni mwa wachezaji waliotarajiwa kupiga pesa za maana katika  dirisha dogo la usajili mwezi uliopita, lakini mambo yalikwenda ndivyo sivyo na kuendelea kubaki katika kikosi cha timu hiyo. Ame ameonyesha uwezo mkubwa wa kufunga mabao kwani katika mechi saba za awali za ligi alikuwa amefunga mabao manne. Baada ya mafanikio hayo Ame ameendelea kutulia na maisha ya Mtibwa na tayari amefunga bao lake la tano katika mechi tisa alizocheza. Mzaliwa huyo wa Zanzibar hana papara na anaonekana kukomaa na kazi yake ya upachikaji wa mabao ili aweze kuzivutia timu nyingi zaidi mwisho wa msimu. Ame anatajwa kuwa miongoni mwa mastaa watakaopiga mkwanja wa maana mwisho wa msimu.
Rashid Mandawa, Kagera
Straika wa Kagera Sugar, Rashid Mandawa huenda akafuata nyayo za mastaa kadhaa waliopita klabuni hapo kama Mrisho Ngassa, Amri Kiemba na Themi Felix kwa kuchota fedha za maana katika usajili wa mwisho wa msimu. Straika huyo ameonekana kuwa moto msimu huu akiwa amefunga mabao matano katika mechi 10 alizoichezea Kagera. Mandawa pia alifanikiwa kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Novemba na kuwapiku mastaa kadhaa wanaoshiriki ligi hiyo. Utulivu wake uwanjani, mwili wake wenye nguvu na uwezo wake wa kumiliki mpira huenda ukazitoa udenda timu kadhaa za ligi kuu na kumsajili kwa dau la maana mwisho wa msimu.

No comments