Hii ndio siri ya utajiri mkubwa wa Manchester United..



MAJANGA yote hayajaitikisa kifedha Manchester United baada ya kutajwa kwamba inashika namba mbili kwenye orodha ya klabu tajiri duniani.
Man United iliyotoka kwenye msimu mbaya ulioshuhudia Kocha David Moyes akifutwa kazi na timu kushindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kumaliza nafasi ya saba kwenye ligi.  Lakini bado imekamata namba mbili kwa klabu matajiri katika orodha iliyotolewa na Deloitte.
Miamba hiyo ya Old Trafford imewapiga kumbo Bayern Munich na Barcelona baada ya mapato yao kupanda kutoka Pauni 363.2 milioni hadi Pauni 433.2 milioni.
Man United ilipata mapato mengi katika msimu wa 2013-14 kuliko klabu nyingine yoyote ya Uingereza na hivyo kuwa namba mbili nyuma ya Real Madrid.
Real Madrid, ambao ni mabingwa wa Ulaya ndiyo klabu matajiri zaidi duniani kwa sasa baada ya kuvuna Pauni 456.5 milioni . Manchester City ni ya pili kwa utajiri kwa klabu za England, lakini duniani inashika namba sita nyuma ya Paris Saint Germain.
Vinara wa Ligi Kuu England, Chelsea inashika nafasi ya saba, Arsenal ipo namba nane na Liverpool ikishika namba tisa na kuzipiku Juventus, Borussia Dortmund na AC Milan.
Klabu 10 matajiri duniani; Real Madrid (Pauni 459.5m), Man United (Pauni 433.2m), Bayern Munich (Pauni 407.7m) na Barcelona (Pauni 405.2m).
Zinazofuata ni PSG (Pauni 396.5m), Man City (Pauni 346.5m), Chelsea (Pauni 324.4m), Arsenal (Pauni 300.5m), Liverpool (Pauni 255.8m) na Juventus (Pauni 233.6m).

No comments