AMISSI Tambwe amepagawa na viwango vinavyoonyeshwa na mastraika
wenzake katika kikosi cha Yanga na amekiri wanampa wakati mgumu wa kujua
afanye nini cha ziada ili kujihakikishia namba kikosi cha kwanza.
Mrundi huyo ameliambia Mwanaspoti kuwa
anashangazwa na uwezo unaoonyeshwa na wenzake hasa Mliberia Kpah Sherman
na wazawa; Danny Mrwanda na Jerry Tegete, anaosema wamekuwa na mazoezi
ya hali ya juu siku chache tangu watolewe katika Kombe la Mapinduzi.
Alisema: “Mastraika wenzangu wananipa changamoto
kubwa kikosini, wanafanya vizuri kila siku hivyo wananipa wakati mgumu
kumshawishi kocha kuwa mimi ndiye straika bora kuliko wao. Sijui nifanye
nini ili kuweza kuwa juu yao.
“Najua natakiwa kujituma zaidi, lakini mchuano ni
mkali na kama kocha akiamua kumtumia mmoja wetu tu kikosini hapo, hali
ndiyo itakuwa mbaya zaidi, tuna ushidani mkali hata mazoezini.”
Tambwe ambaye alisajiliwa Yanga Desemba mwaka jana
baada ya kutemwa na Simba, alisema tofauti na timu nyingine, mastraika
kikosini hapo kila mmoja ni mpambanaji na ana uchu wa kufunga kuanzia
mazoezini hadi kwenye mechi.
“Wote kuanzia Sherman, Mrwanda na Tegete wanacheza
soka la hali ya juu. Nina uhakika kocha atakuwa anaumiza akili yupi wa
kumpanga na yupi wa kumweka nje, hakika hapa natakiwa kufanya kazi ya
ziada vinginevyo mambo yatakuwa magumu,” alisema.
“Lakini ushindani huu unatufanya tuwe na timu imara, siyo siri timu itakayokutana na sisi tutaiangushia kipigo kikubwa.”
Jumamosi Tambwe anaweza kuichezea Yanga dhidi ya
Ruvu Shooting katika mwendelezo wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam.
Msimu uliopita Tambwe alipoichezea Simba dhidi ya
Ruvu, alifunga mabao mawili timu yake ikishinda 3-2. Yanga iliifunga
Ruvu mabao 7-0.
Post a Comment