KIPA Ivo Mapunda hivi karibuni alitangaza kutoichezea Simba katika mechi zozote kwa kuwa kila anapofungwa analaumiwa.
Lakini akiwashangaza wengi, juzi Jumanne usiku
katika fainali ya Kombe la Mapinduzi aliingia uwanjani katika dakika ya
90 na kupangua penalti moja iliyoipa ubingwa timu yake.
Baada ya mechi hiyo, Mapunda aliliambia Mwanaspoti
kuwa alishindwa kukataa kuingia kuchukua nafasi ya Manyika Peter kwani
Kocha Goran Kopunovic alimshtukiza kumpa nafasi hiyo na hakuweza kukataa
kutokana na hali halisi.
Baada ya kuona mechi ya fainali ya Kombe la
Mapinduzi dhidi ya Mtibwa Sugar inaelekea katika mikwaju ya penalti,
Kopunovic alimwingiza Mapunda ambaye alifanikiwa kupangua penalti ya
mwisho ya Vincent Barnabas na kuipa Simba ushindi wa penalti 4-3.
“Kweli nilisema sitaichezea tena Simba baada ya
maneno kuwa mengi kwamba nafungisha, nilicheza na Mtibwa kwa sababu
kilikuwa kitu cha ghafla ambacho kocha aliniambia nami nikajikuta
nimesimama na kwenda uwanjani,” alisema.
“Kweli kama ningefanya vibaya pale hali ingekuwa mbaya zaidi, ningeonekana nimefungisha, lakini namshukuru Mungu.”
Alipoulizwa kama msimamo wake bado uko palepale, Mapunda alishindwa kufafanua zaidi.
Mapunda hakucheza mechi yoyote ya michuano hiyo awali na ameweka rekodi ya kipa aliyecheza kwa muda mfupi michuano hiyo.
Akizungumzia uhodari wake wa katika penalti,
Mapunda alisema alimchanganya kisaikolojia kiungo wa Mtibwa Sugar,
Ibrahim Rajabu ‘Jeba’, kwa kutompa mpira uliokuwa wavuni. “Mpira una
mambo mengi, nilifanya makusudi kutompa mpira Jeba kwa lengo la kumtoa
mchezoni, kweli alitoka mchezoni ndiyo maana alikosa penalti kwa
kugongesha mwamba.”
Post a Comment