KLABU ya Arsenal imepanga kutuma maofisa biashara wake jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili fursa za ushirikiano na wafanyabiashara kadhaa wakubwa wa nchini.
Huu utakuwa ujumbe wa kwanza kabisa wa Arsenal
nchini Tanzania ambapo klabu hii kubwa ya Ligi Kuu England inataka
kujenga ushirika katika maeneo ya masoko na chapa zake, ili kutanua
mafanikio yaliyofikiwa kwenye nchi nyingine za Afrika zikiwamo Kenya,
Uganda na Nigeria.
Arsenal inataka kutoa fursa kwa benki za Tanzania
pamoja na kampuni za simu na taasisi nyingine kuweza kupata rasilimali
zihusianazo na klabu hiyo ya London, kama vile bidhaa zilizosainiwa kwa
majina ya wachezaji na tiketi za mechi zao za soka.
Ofisa Biashara Mkuu wa Arsenal, Vinai Venkatesham,
alisema wameichagua Tanzania kwa sababu wana washabiki wengi na kwa
kushirikiana na taasisi za hapa, watakuwa karibu zaidi na mashabiki wao
kuliko ilivyokuwa awali.
“Katika bara lenye nchi zaidi ya 50, tumechagua kuzuru Tanzania kimkakati kwa sababu tunaiamini nchi hii,” alisema.
“Arsenal ina mamilioni ya Watanzania ambao ni
washabiki waaminifu na wenye mapenzi makubwa nayo, hivyo kwa
kushirikiana na taasisi za hapa, tutaweza kuisogeza klabu karibu zaidi
na mashabiki.”
Wajumbe hao wa jopo la Maendeleo ya Ushirikiano ya
Arsenal wanatarajia kuwasili nchini Januari 18 na kukaa kwa wiki moja
jijini Dar es Salaam, wakiitisha mikutano kadhaa na wafanyabiashara.
Ujio wa viongozi wa timu hiyo umeratibiwa na
kampuni ya EAG Group Tanzania ambapo Ofisa Mtendaji Mkuu wake, Imani
Kajula alisema: “Ujio huu utainufaisha zaidi Tanzania kukua katika sekta
mbalimbali.”
Post a Comment