Straika aikimbia Yanga.



YANGA na Simba kwa nyakati tofauti zimefanya mazungumzo ya awali na straika wa JKU ya Zanzibar, Amour Mohammed ‘Janja’ ambaye ni Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Zanzibar akiwa na mabao manane, lakini mwenyewe amewapiga chenga ya mwili na kutua Azam.
Timu hizo zilitaka kumwandaa mchezaji kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, lakini amechomoa kwa madai kwamba anazijua sana klabu hizo hivyo hawezi kuingia mkenge. Janja, mpaka JKU inatolewa kwenye nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi alikuwa na mabao mabao matatu akimfuatia Simon Msuva aliyepachika manne.
Janja alisema awali mmoja wa viongozi wa Simba alimfuata mapema akitaka kujua kama yupo tayari kujiunga na timu hiyo, lakini pia kocha wake Malale Hamsini amemwambia kwamba Yanga wanamtaka.
Alisema kwa sasa chaguo lake ni kukipiga na Azam ambayo ndiyo klabu tajiri zaidi kwa sasa Afrika Mashariki.
“Unajua mimi nazijua hizi timu kubwa, hazina subira, nawashukuru kwa kuonyesha kunihitaji, lakini ningekuwa na uwezo ningewaambia Azam waje wanisajili kuliko Simba na Yanga,”alisema Janja.
“Azam ndiyo chaguo langu, klabu yao wanaiendesha kwa malengo sana hakuna matatizo kama ya Simba na Yanga wanajua kumthamini mchezaji.”

No comments