Sasa ndiyo mtauona utamu wa Simba





SIMBA ni kama wanawakebehi watani wao Yanga ambao juzi Alhamisi waliondoshwa kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi na JKU ya Zanzibar.
Unajua Msimbazi wamesemaje? Wamesema wao hawana lelemama na watakomaa na kuhakikisha wanatinga fainali na kutwaa taji.
Simba ilifanikiwa kutinga nusu fainali ya mashindano hayo mapema Jumatano baada ya kuifunga Taifa Jang’ombe mabao 4-0 na leo Jumamosi inacheza na Polisi Zanzibar kusaka tiketi ya fainali.
Polisi wao walitinga hatua hiyo baada ya kuwavua ubingwa KCCA ya Uganda kwa penalti 5-4 baada ya matokeo ya suluhu ndani ya dakika 90.
Nusu fainali nyingine itakuwa kati ya Mtibwa Sugar na wababe wa Yanga ambao ni JKU, utakuwa kama marudio ya ule wa hatua ya makundi uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.
Mtibwa imetinga hatua hiyo baada ya kuifunga Azam kwa penalti 7-6 baada ya sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90 wakati JKU wao waliifunga Yangao bao 1-0. Mechi zote zitachezwa Uwanja wa Amaan.
Kocha wa Simba, Goran Kopunovic alisema ameshtushwa na kitendo cha Azam na Yanga kuondoshwa katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo lakini amewaambia wachezaji wake kuwa wakomae na kuupa uzito mchezo huo ili waweze kutinga fainali na kutwaa taji hilo.
“Tunaingia kwa akili moja ya kutengeneza nafasi na kuzitumia, tunaingia kwa umakini mkubwa, tumedhamiria kutinga fainali na kutwaa taji hili,” alisema kocha huyo.
Naye kocha wa Mtibwa, Mecky Maxime, amesema hatma ya mchezo wao wa leo na JKU iko mikoni mwa wachezaji wake kwani wanafahamu ni kitu gani wanatakiwa kukifanya uwanjani ndani ya dakika 90 za mchezo huo.
“Tulimaliza maandalizi ya mechi hizi tangu tuko kwetu Morogoro, tumekuja huku kucheza na wachezaji wangu wanafahamu kuwa tunahitaji nini, tunawafahamu JKU na tulicheza nao kwenye mchezo wa makundi, ni timu nzuri na upinzani utakuwa mkubwa,” alisema Maxime.
Ligi Kuu Bara
Kwenye mechi za Ligi Kuu Bara leo Jumamosi Ndanda FC ya Mtwara itaikaribisha Polisi Morogoro kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

No comments