Sasa Yanga ni full raha
MASHABIKI wa Yanga jana Jumatano walikuwa na furaha kuliko wale wa Mbeya City ambao timu yao iliifunga Simba mabao 2-1 katika mechi ya Ligi Kuu Bara pale Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ipo hivi; mashabiki wa Yanga wanaamini kufanya
vibaya kwa Simba ni neema katika harakati zao za kutwaa ubingwa wa ligi
hiyo msimu huu.
Kwa ushindi ilioupata, Mbeya City imepanda mpaka
nafasi ya saba kutoka ya 12 ikiwa na pointi 15 huku Simba ikishuka hadi
nafasi ya 11 kutoka ya kumi, imebaki na pointi 13 zake.
Mchezo wa jana ulijaa upinzani mkali kutokana na
rekodi za timu hizo msimu uliopita ambapo katika mechi ya kwanza timu
hizo zilitoka sare ya bao 1-1 pamoja na 2-2.
Hadi ilipoingia dakika ya 90 jana, timu hizo
zilikuwa sare kwa bao 1-1 na tayari baadhi ya mashabiki walishaanza
kutoka uwanjani wakiamini mchezo ungemalizika kwa sare hiyo, kabla ya
mambo kubadilika kwenye dakika za majeruhi ambapo Watoto wa Mbeya
wakashinda kwa bao la penalti.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha wa Mbeya
City, Juma Mwambusi alisema: “Mwanzo wachezaji wangu hawakuwa makini,
lakini tulipoenda mapumziko niliwataka watulie na kuwaeleza tatizo la
Simba, nashukuru walifanya nilivyotaka. Lakini mwamuzi aliipa Simba
penalti isiyo halali lakini pia nashukuru wakakosa, sasa tunatazama
mechi zijazo.”
Naye Kocha wa Simba, Goran Kopunovic alisema:
“Kilichotuponza katika mechi hii ni kuridhika na bao moja la kuongoza
ndiyo maana nikawatoa akina Sserunkuma (Dan na Simon), lakini bado
hawakuweza kupambana kuongeza bao lingine.”
Awali Simba ilianza mchezo kwa kasi na kutawala
sehemu ya kiungo ambapo Jonas Mkude alimzidi uwezo kiungo mkongwe wa
Mbeya City, Steven Mazanda. Uwezo huo wa Simba uliiwezesha kupata bao
dakika ya 23 lililofungwa na Ibrahim Ajib kwa faulo iliyopigwa nje
kidogo ya eneo la hatari. Faulo hiyo ilitolewa na mwamuzi Abdallah
Kambuzi wa Shinyanga baada ya Awadh Juma kuchezewa vibaya na Hamad
Kibopile.
Katika dakika za 25 na 35 timu zote zilipoteza
nafasi, ilianza Simba pale Ramadhan Singano alipopiga nje kabla ya Paul
Nonga kupanguliwa kiki yake na kipa wa Simba, Manyika Peter.
Kipindi cha pili Simba iliwatoa Dan Sserunkuma,
Ajib na Simon Sserunkuma na nafasi zao kuchukuliwa na Elius Maguli, Abdi
Banda na Ibrahim Twaha.
Post a Comment