Pluijm ajaribu kutumia mbinu mpya Yanga



KOCHA Mkuu wa Yanga, Mholanzi Hans Pluijm, ameanza staili mpya kuwapa wachezaji mazoezi ya uwanja mdogo ili kuwatoa woga kila wanapoingia ndani ya 18.
Kocha huyo ambaye kikosi chake kiliifunga Polisi Morogoro bao 1-0 Uwanja wa Jamhuri huku washambuliaji wake wakipoteza nafasi nyingi, alisema:  “Tunacheza mechi ijayo hapa Dar es Salaam na mazingira ya uwanja ni mazuri.
“Lakini kama unavyoona katika maandalizi yetu mazoezini, kuna vitu tunafanya kwa ajili ya kukabiliana na tatizo hilo.
“Kama ulivyoona tunafanya mazoezi kwa kutumia nafasi ndogo ya uwanja, lengo ni kuwafanya wacheze kwa kujiamini, haraka na utulivu kwa pasi za kueleweka kila wanapofika ndani ya 18 na waweze kufunga.
“Na kwa hali hiyo, natarajia kupata matokeo yenye mabao mengi zaidi kwa sababu ya mbinu hiyo.
“Unajua kwa sasa ligi imeshakuwa na ushindani mkubwa hivyo hatupaswi kuendelea kupoteza nafasi mchezoni.”
Katika mazoezi hayo ya juzi Jumanne ambayo walifanya kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe, jijini Dar es Salaam, Pluijm alitumia sehemu ndogo na kuwaeleza mbinu mbalimbali.
Imeonekana namna ambavyo Yanga inafanya mashambulizi mazuri na kufika ndani ya 18 lakini wanakosa umakini na kufanya mipira hiyo kuokolewa na mabeki au kupaisha angani tatizo ambalo linasababishwa na ukosefu wa kujiamini.
Yanga inarudi uwanjani Jumapili ijayo kukipiga na Ndanda Uwanja wa Taifa na baada ya hapo itaelekea Tanga kuwavaa Coastal Union kabla ya mechi yao na BDF ya Botswana.

No comments