Sasa Simba waamua kufanya uamuzi mgumu



WAZEE wa Simba wameona isiwe taabu na wameamua kurudi kazini kwa kufanya kikao chao cha dharura na baadhi ya viongozi na jana Alhamisi jioni walituma ujumbe wao kambini kuzungumza na wachezaji kwenye kikao cha faragha kutaka kujua tatizo ni nini mbona timu inayumba?
Lakini si hilo tu, viongozi wa matawi ya Simba Dar es Salaam wameungana na kuuandikia barua uongozi wakishinikiza mambo matatu ambayo ni uamuzi mgumu, ambayo ni kuitisha mkutano wa dharura wa wanachama kujua tatizo la timu yao, kufumua benchi la ufundi abaki kocha Mserbia, Goran Kopunovic pekee na mwisho Kamati ya Mashindano ipigwe chini.
Wanachama hao chini ya kiongozi wao, Masoud Ustaadh, wanadai kwamba mambo hayo ndiyo tatizo na chanzo cha Simba kufanya vibaya kwenye Ligi Kuu Bara na kwamba viongozi wa kamati wamekuwa wakiingilia benchi la ufundi.
Kwa mujibu wa maelezo yao, wanataka hata Selemani Matola apigwe chini kwa madai kwamba hata Kocha Patrick Phiri alishadokeza awali kuwa Kocha Msaidizi huyo hafai.
Rais wa Simba, Evans Aveva, amekiri kupokea barua hiyo na kusema anaifanyia kazi kwa mujibu wa Katiba ya Simba.
Tafrani hiyo imezuka baada ya timu hiyo kupigwa mabao 2-1 na Mbeya City juzi Jumatano kwenye mechi ya ligi hiyo  ndani ya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wazee hao waliibukia kambini jana kutaka wachezaji wawaambie ukweli ambapo kikao hicho kilitumia saa kadhaa huku kukiwa na usiri mkubwa.
Mmoja wa wachezaji aliiambia Mwanaspoti baadaye kwamba baadhi yao walitamka kwamba walifungwa kwa makosa ya uwanjani, ingawa wengine walilalamika kuwa morali iko chini kwavile viongozi hawapo karibu nao.
Kocha aliyetimuliwa na Simba, Patrick Phiri kwa upande wake ameweka wazi kwamba timu hiyo ilikosea kuwaacha Amri Kiemba na Haroun Chanongo lakini akatoa angalizo kwamba Mserbia Kopunovic asiguswe, aachwe afanya kazi yake.
Phiri alitimuliwa Simba mwezi uliopita na nafasi yake kuchukuliwa na Mserbia huyo.
Akizungumza na Mwanaspoti jana kutoka Zambia, Phiri alionyesha kusikitishwa na matokeo ya Simba lakini akasema: “Bado uwepo wa Chanongo na Kiemba ndani ya Simba ulikuwa muhimu sana, kila mchezaji ana udhaifu wake kama binadamu,  lakini viongozi wanapaswa kukaa na wachezaji kuzungumza nao kujua matatizo yao.”
Kiemba alijiunga na Azam kwa mkopo kama Chanongo alivyokwenda Stand United ya Shinyanga.

No comments