Ngassa atoroka Yanga
YANGA imetenga Sh168 milioni kwa ajili ya mechi mbili za awali
za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya BDF XI ya Botswana itakayochezwa
Februari 14, lakini Mrisho Ngassa ametorokea Afrika Kusini kufanya
majaribio ya soka la kulipwa.
Ngassa ambaye amewahi kuzichezea Simba, Azam na
Kagera Sugar, amekosekana katika timu hiyo kwa wiki moja sasa ambapo
uongozi unaeleza kwamba anamuuguza ndugu yake ambaye maelezo yake
hayajawekwa wazi.
Lakini Mwanaspoti lina habari kwamba mchezaji huyo
aliyewahi kutakiwa na Westham ya England pamoja na El Merreikh ya
Sudan, yupo Afrika Kusini akifanya majaribio na klabu ya Free State
Stars ambayo imekuwa ikimfuatilia kwa kipindi kirefu na wakala mmoja
tajiri nchini Tanzania ndiye aliyemuunganisha na timu hiyo.
Mtendaji Mkuu wa shughuli za kila siku za Yanga
ambaye ni Katibu Mkuu, Jonas Tibohora, alisema Ngassa aliondoka akiomba
ruhusa maalum ya kumuuguza ndugu yake, lakini uongozi kupitia vyanzo
vyake umepata taarifa kwamba yuko Afrika Kusini akisaka timu ya
kumsajili bila ya ruhusa.
Tibohora ambaye kitaaluma ni daktari wa Sayansi ya
Michezo, alisema taarifa hizo wamezipata kutoka kwa baadhi ya wadau wa
klabu yao ambao wamemuona mshambuliaji huyo nchini humo huku klabu
inayotajwa kwamba ndiyo inataka kumsajili ni Free State Stars ambayo
iliwahi kumfanyia majaribio mwaka jana.
Alisema kwa sasa wanaendelea na uchunguzi wa hilo
akisema endapo watabaini ukweli katika utovu huo wa nidhamu wa
mshambuliaji huyo, atakaporudi watakutana naye huku akidokeza uwezekano
wa kuishitaki Free State Stars.
“Alikuja kwangu akaomba ruhusa kwamba anamuuguza
ndugu yake, kibinadamu hatukuweza kumzuia tukamkubalia, lakini taarifa
tulizopata ni kwamba hayuko nchini kitu ambacho kilitushtua na hata
tulipokuwa tunamtafuta kutaka kujua maendeleo ya mgonjwa wake hatukuwa
tunampata,”alisema Tibohora.
“Awali nilimshtukia Ngassa wakati anaomba ruhusa
alitaka pia tumpatie barua ya kwenda kushughulikia pasi yake ya
kusafiria, nilijiuliza kuna uhusiano gani kati ya mgonjwa na pasi ya
kusafiria sikupata majibu tunaendelea na uchunguzi wa hilo,”alisisitiza
kiongozi huyo ambaye klabu yake inakabiliwa na mechi mbili za Ligi Kuu
Bara dhidi ya Ndanda na Mtibwa kabla ya kuingia kwenye michuano ya
kimataifa.
YATENGA SH168 MILIONI
Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata
wikiendi iliyopita ni kwamba Yanga imetenga Sh168 milioni katika Kombe
la Shirikisho Afrika dhidi ya BDF XI ya Botswana.
Yanga imepanga kutumia Sh36 milioni katika
maandalizi ya mchezo wa kwanza dhidi ya BDF utakaochezwa nchini Februari
14 na itatumia dola 78,000 (Sh132 milioni) katika mchezo wa marudiano
utakaochezwa Botswana wiki mbili baadaye.
Msimu uliopita wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga
iliweka bajeti ya dola 78,000 pia ili kuivaa Al Ahly ya Misri katika
mchezo wa marudiano uliochezwa Misri.Hata hivyo Yanga ilitolewa na Al
Ahly kwa penalti 4-3 baada ya kufungwa bao 1-0 huku wakiwa wameshinda
bao 1-0 nyumbani.
Post a Comment