Yanga yagundua utofauti kwa Dida na Barthez


KAMA ulikuwa hujui siri ya Yanga kumtumia kipa wake, Ally Mustapha ‘Barthez’ katika mechi za sasa, basi fahamu kuwa lengo ni kumweka sawa ili awe kwenye kiwango cha juu kama ilivyo kwa Deo Munishi ‘Dida’.
Hiyo ni baada ya kugundua wanakabiliwa na mechi ngumu za Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho ambapo wataanza na BDF ya Botswana.
Yanga inaamini kama, Dida na Barthez wote watakuwa kwenye kiwango cha juu, ni faida kwa timu lakini kama mmoja wao atakuwa juu na mwingine atakuwa hayuko sawa, inaweza kukiathiri kikosi endapo huyo wanayemtegemea akipata matatizo.
Kocha wa makipa wa Yanga, Juma Pondamali ameliambia Mwanaspoti akisema: “Kwa sasa huwezi kutofautisha kiwango cha Dida na Barthez wote wapo vizuri na viwango vyao vinafanana.
“Kwa sasa tunamtumia Barthez, ni mipango tu. Lengo ni kuwaweka vizuri makipa wetu wote, kama unavyojua tuna mechi ngumu mbele yetu kama za ligi na michuano ya Afrika , wote wanatakiwa kuwa vizuri.
“Hii itatusaidia kufanya chaguo lolote kulingana na mchezo husika, sasa kama kutakuwa na tofauti mmoja yuko kwenye kiwango cha juu na mwingine hayuko vizuri na kisha kukatokea tatizo kwa huyo anayetegemewa kama vile akaumwa au akapata shida nyingine yoyote, itakuwa balaa kwenye timu.”
Katika msimu huu wa ligi, awali Yanga ilikuwa ikimtumia Dida katika mechi zake, lakini sasa imekuwa tofauti baada ya Barthez kuanza kupewa nafasi ya kucheza kama ilivyo kwa mwenzake.

No comments